Featured Kitaifa

WANANCHI WAACHE KUNUNUA MAJOKOFU, VIYOYONZI MTUMBA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi Ofisi Ya Makamu Wa Rais (Muungano Na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati akitoa Tamko kuhusu kuelekea Siku ya Maadhimisho ya  Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni yanayotarajia kufanyika Septemba 16, 2023

………………………

Serikali imewataka wananchi kuepuka kuingiza nchini na kutumia majokofu au viyoyozi vilivyokiwshatumika (mtumba) ambavyo vinatumia gesi haribifu kwa tabaka la ozoni na badala yake watumie bidhaa zenye uwezo mdogo wa kuchangia ongezeko la joto duniani.

Waziri wa Nchi Ofisi Ya Makamu Wa Rais (Muungano Na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema hayo wakati akitoa Tamko kuhusu Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni jijini Dodoma leo Septemba 13, 2023.

Amesema hayo wakati Tanzania ikitarajia kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni Septemba 16, 2023 kama kumbukumbu ya tarehe ya kutiwa saini Itifaki ya Montreal ya mwaka 1987 kuhusu kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni ambalo kazi yake kubwa ni kuchuja sehemu kubwa ya mionzi ya jua isifike kwenye uso wa dunia. 

Akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa katika utekelezaji wa Mkataba wa Montreal Serikali ilitoa mafunzo kwa maafisa wa mipakani kuwa kutambua vifaa vinavyotumia kemikali haribifu kwa tabaka la ozoni ambalo linapoharibiwa huruhusu mionzi ya jua kufika kwenye uso wa dunia na hivyo kusababisha madhara.

Dkt. Jafo alisema tabaka la ozoni linapoharibiwa husababisha saratani ya ngozi, mtoto wa jicho, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi, kujikunja kwa ngozi, kuathirika kwa ukuaji wa mimea pamoja na kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi.

Hivyo, alitoa wito kwa wananchi kununua bidhaa zilizowekwa nembo rasmi isemayo “Ozone friendly” au “low global warming potential” au  yaani “sahibu wa Ozoni” au “uwezo mdogo wa kuchangia ongezeko la joto duniani”. 

Madhara mengine aliyataja kuwa ni kuathirika kwa ukuaji wa mimea vile vile, baadhi ya kemikali hizi husababisha kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi.

 

“Ukiangalia mwaka juzi kuna kazi mbalimbali zilikuwa zikifanyika kwa mafundi wa majokofu na kwenda katika maduka ili kuhamasisha na kutoa mafunzo kwa mafundi ili waweze kujua madhara yake,” alisema Jafo.

 

Mafunzo hayo yalilenga namna ya kudhibiti uingizaji wa kemikali nchini kwa Maafisa wa Idara za Serikali zilizopo katika Mpaka wa Namanga na kutoa elimu kwa wanafunzi wa fani ya viyoyozi katika Chuo cha Ufundi Arusha pamoja na mafundi wa viyoyozi na majokofu kwa mkoa wa Arusha kuhusu namna bora ya kukarabati vifaa hivyo pasipo kuachia angani kemikali na hivyo kuharibu mazingira.

  

Kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni mwaka huu ni “Hifadhi ya tabaka la ozoni na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi” ambayo imechaguliwa kutokana na mafanikio ya kimataifa kupitia utekelezaji wa Itifaki ya Montreal katika kuchangia jitihada za kuhifadhi tabaka la ozoni na kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.

About the author

mzalendoeditor