Featured Kitaifa

TBS YATOA ELIMU KWA WANANCHI 2,276

Written by mzalendoeditor
Na Mwandishi Wetu
 
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) imetoa elimu kwa wananchi 2,276 kupitia kampeni yake ya kutoa elimu kwa umma katika Halmashauri ya Wilaya za Malinyi , Ulanga, Gairo na Mvomero mkoani Morogoro juu ya umuhimu wa kusoma taarifa zilizopo katika bidhaa, kununua bidhaa zilizothibitishwa na shirika hilo, sambamba na kuwahamasisha wajasiriamali wadogo kuthibitisha ubora wa bidhaa zao na wafanyabiashara kusajili maduka ya chakula na vipodozi.
 
Kampeni hiyo ya elimu kwa umma ambayo ilianza tarehe 21 mwezi wa nane na kuhitimishwa tarehe 5 mwezi wa tisa mwaka huu katika wilaya hizo imefanyika katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya masoko, stendi, minadani na maeneo mengine ya wazi, ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi kupata elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali yahusuyo ubora wa bidhaa.
 
Kupitia kampeni hiyo wajasiriamali waliofikiwa na elimu hiyo ni 118 na wananchi 2158 na kufanya jumla yao 2,276.
 
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ulanga, Andreas Whero aliipongeza TBS kwa kutoa elimu kwa wananchi na alishauri kufanya kaguzi za kushtukiza mara kwa mara madukani hususani katika bidhaa za ujenzi kama nondo na mabati sambamba na kutumia redio jamii za wilayani ili kufikia wananchi wengi zaidi.
 
Akizungumza wakati wa Kampeni hiyo, Meneja Wa Uhusiano na Masoko TBS, Gladness Kaseka, alisema lengo la Shirika hilo ni kutoa elimu kwa umma katika ngazi za wilaya zote.
 
” Kwa sasa TBS tumeamua kuwafikia wajasiriamali, wafanyabiashara na wananchi katika ngazi za wilaya ili kuwapatia utaratibu unaotakiwa kwa ajili ya kupata alama ya ubora na kusajili majengo ya biashara ya chakula na vipodozi ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza, kwa hiyo elimu hii ya umma ipo katika ngazi ya wilaya na hadi sasa TBS imezifikia wilaya 63 ,” alisema Kaseka
 
Nao wajasiriamali kutoka vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Malinyi waliipongeza TBS kwa elimu waliyoitoa maana imewafumbua mambo mengi kuhusu umuhimu wa viwango katika bidhaa wanazozizalisha.
 
Kwa upande wake Mkaguzi TBS, Kaiza Kilango aliwakumbusha wananchi kutambua kuwa vita ya bidhaa hafifu sio ya shirika hilo pekee, bali ni ya Taifa kwa ujumla na hivyo wasisite kutoa taarifa pindi wanapokutana na bidhaa zilizokwisha muda wake au wanapotilia shaka bidhaa yoyote katika soko.
 
Kaiza aliwafafanulia wananchi umuhimu wa viwango katika maisha yao ya kila siku vile vile kuwafahamisha fursa ya huduma bure kwa wajasiriamali wadogo.
 
Aliwataka wawe mabalozi wa kuhamasisha ubora katika jamii wanazoishi.
 
Aidha, aliwataka wafanyabiashara kufuatilia taratibu sahihi za usajili wa bidhaa au majengo ya chakula na vipodozi kwa kutembelea ofisi ya TBS iliyopo karibu au kupiga katika kituo cha huduma kupitia mawasiliano yaliyotolewa.
 
Kampeni ya kuelimisha umma ni endelevu na itaendelea katika wilaya za mkoa wa Tabora , Mtwara na Lindi.

About the author

mzalendoeditor