Featured Kitaifa

KIGOMA UJIJI KUPIMA NA KUSAJILI MAKAZI 10,000 KATIKA MITAA 25.

Written by mzalendoeditor

 Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe. Salum Kalli ,akizungumza wakati akifungua Mkutano wa wadau wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milko za Ardhi nchini unaotekelezwa Manispaa ya Kigoma Ujiji leo Septemba 4,2023.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Bw.Evans Mdee,akizungumza wakati wa  Mkutano wa wadau wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milko za Ardhi nchini unaotekelezwa Manispaa ya Kigoma Ujiji leo Septemba 4,2023.

Sehemu ya washiriki wakifatilia hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe. Salum Kalli (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano wa wadau wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milko za Ardhi nchini unaotekelezwa Manispaa ya Kigoma Ujiji leo Septemba 4,2023.

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe. Salum Kalli,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua  Mkutano wa wadau wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milko za Ardhi nchini unaotekelezwa Manispaa ya Kigoma Ujiji leo Septemba 4,2023.

Na.Alex Sonna

WADAU wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini wamekutana kujadili namna ya kuondokana na ongezeko la idadi ya  ukuaji wa makazi yasiyopangwa huku wakiitaka Manispaa ya Kigoma Ujiji kuuchukua mradi huo kama fursa  na kutoa ushirikiano thabiti ili kufanikisha utekelezaji wake.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika Kigoma Ujiji leo Septemba 4,2023 Mkuu wa wilaya ya Kigoma Mhe. Salum Kalli ,amesema Mradi huo umelenga kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kupanga, kupima na kusajili milki za ardhi zipatazo milioni 2.5 .

Amesema milki hizo zinatajumuisha hati milki 1,000,000 na Leseni za Makazi 1,000,000 katika maeneo ya mijini na Hati za Hakimilki za Kimila 500,000 vijijini; ambapo Manispaa ya Kigoma Ujiji  inakusudia kupanga, kupima na kusajili makazi 10,000 katika mitaa 25.

“Nchi yetu ina jumla ya Halmashauri 185 Kati ya Halmashauri hizo, Halmashauri 41 ndio zinazotarajiwa kunufaika na mradi huu,nashauri itumieni fursa hii kikamilifu kwa maendeleo ya Manispaa yetu ya Kigoma Ujiji na Mkoa wetu wa Kigoma kwa ujumla,”amesema.

Aidha amesema Urasimishaji huu wa ardhi katika Manispaa hiyo utaleta matokeo chanya katika kuchochea maendeleo ya Wilaya ikiwa ni pamoja na kuleta usalama wa milki za ardhi, kukukuza uchumi na kupunguza au kumaliza migogoro itokanayo na ardhi.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa  Mradi huo pia umelenga kusimika Mfumo Unganishi wa kielektroniki wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi (ILMIS) katika ofisi zote za Ardhi za Mikoa na Halmashauri mbalimbali.

“Hatua hii ni kwa kuzingatia sera za utandawazi, nchi yetu imeingia makubaliano mbalimbali za kimataifa na za kikanda ili kuendana na kasi ya maendeleo ya Dunia yanayohusisha makubaliano ya kiuchumi, kijamii na kimazingira,

 Makubaliano hayo kwa uchache ni pamoja na Agenda ya Afrika 2063 inayoitaka Afrika kuhakikisha upangaji bora na umiliki wa ardhi, mifumo ya matumizi ya ardhi na usimamizi wa maendeleo sawia ya makazi ya watu katika ngazi zote kuanzia vijijini hadi mijini,”amesisitiza

Mhe.Kalli ameeleza kuwa  Agenda hii pia inaelekeza kuwa, sera zitakazotungwa na kutekelezwa zinatakiwa pamoja na masuala mengine kujikita katika kuchochea usawa katika upatikanaji na umiliki wa ardhi kwa makundi yote katika jamii hususani kwa wanawake na watu wenye mahitaji maalumu.

“Azimio la umoja wa Afrika kuhusu masuala ya ardhi linazitaka nchi wanachama wa umoja wa Afrika kufanya maboresho katika sekta  za ardhi na kuandaa sera madhubuti, inayozingatia mahitaji mahususi ya jamii,changamoto  zote zitakazo jitokeza katika utekelezaji wa Mradi huu utatatuliwa na watanzania wenyewe kwa taratibu za Sheria, Kanuni na Miongozo ya sheria za nchi yetu,”amesisitiza

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Bw.Evans Mdee,amewataka  wadau hao wa ardhi kutumia fursa hiyo  kutoa mawazo na maoni ya kuboresha utekelezaji wa mradi huo ambao ni muhimu kwa Halmashauri hiyo ili kufikia lengo la kuboresha Usalama wa Milki za Ardhi kwa Wananchi .

Amesema Katika Manispaa hiyo utekelezaji wa mradi  ulianza  mwezi Juni, 2023 ikiwa na lengo la kutambua, kupanga, kupima na kusajili milki zipatazo 10,000 ambazo zitamilikishwa kwa wananchi wa Manispaa ya Kigoma.

“ Kazi ambazo zimefanyika ni pamoja na kutambulisha mradi kwa wajumbe wa menejimenti ya Halmashauri (CMT) na baraza la Madiwani,tiimu za wataalam wa Manispaa ya Kigoma wametoa elimu kwa viongozi wa Kamati ya maendeleo ya Kata za Kibirizi, Kasingirima na Kagera na wamefanya mikutano ya hadhara ya mitaa kumi katika Kata za Kibirizi, Kasingirima na Kagera,”amesema Bw.Mdee

Aidha, amesema hadi sasa zaidi ya makazi 4,000 yametambuliwa katika Kata ya Kibirizi, michoro ya viwanja 1,500 imeandaliwa na wananchi wa Mtaa wa Kibirizi wanaendelea kuhakiki taarifa zao za umiliki na kazi inaendelea.

About the author

mzalendoeditor