MBUNGE wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota,akiulizwa swali leo Agosti 29,2023 bungeni jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu Dodoma
MBUNGE wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota ameiomba serikali kuwafikia wakulima wengi wa zao la korosho huku kutakuwa na kiuatilifu kimoja cha magonjwa kwenye zao hilo ili kuondokana na utitiri wa viuatilifu ulipo.
Akiuliza swali bungeni leo, Chikota amesema kumekuwapo na utitiri wa viuatilifu kwenye zao hilo na kuhoji serikali haioni umuhimu wa kutoa elimu kwa wakulima wakati wa kugawa viuatilifu hivyo.
“Naipongeza serikali kwa kusajili wakulima ili kutoa pembejeo na viuatilifu lakini kuna kundi kubwa la wakulima hadi sasa hawajasajiliwa je, serikali ina mpango gani wa kufanya usajili kwa wakulima hao,”amehoji.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde amesema kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu serikali imeanza kupitia upya usajili na viuatilifu vyote ili kubaki na viuatilifu vinavyofaa sokoni kulingana na aina ya zao, eneo na magonjwa yaliyopo.
Mavunde amesema katika zao hilo kuna magonjwa makuu manne ambayo ni ubwiriunga, blaiti, chule na debeki yanayodhibitiwa kwa viuatilifu vyenye viambata amilifu tofauti.
“Ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa visumbufu vya mazao Serikali itaendelea kuimarisha utafiti na kushauri wakulima kutumia viuatilifu vyenye tija zaidi katika kilimo,”amesema.
Kadhalika, amesema utiriri wa viuatilifu unatokana na magonjwa ya mazao na wadudu waharibifu na kwamba kupitia Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo(TARI) Naliendele na Bodi ya Korosho wataendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya viuatilifu hivyo.
Amekiri kuna wakulima bado hawajasajiliwa na nguvu imeongezwa kupitia Bodi hiyo kuongeza idadi ya rasilimali watu ili kufanikisha kusajili wakulima na wapate viuatilifu kwa wakati.