Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewapongeza Wabunge wa Zanzibar kwa kutumia vyema nafasi zao za uwakilishi wa majimbo yao ambapo juhudi hizo zimewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Dkt. Jafo ameyasema hayo leo Agosti 24, 2023, wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kilichopokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Awamu ya Nane inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Hussein Ally Mwinyi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi imetokana na mshikamano mkubwa unaofanywa na Wabunge wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusemea na kutetea hoja mbalimbali.
“Leo hii ndani ya miaka miwili ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Awamu ya Nane, Mhe. Dkt. Hussein Ally Mwinyi tumeshuhudia mageuzi makubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi…Juhudi hizi zimetokana na ninyi Wabunge katika kujenga hoja Bungeni” amesema Dkt. Jafo.
Waziri Jafo amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeendelea kupokea kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo huku akitolea mfano fedha za miradi ya UVIKO 19 ambazo zimetekeleza miradi ya sekta muhimu za kijamii kwa wananchi ikiwemo afya, elimu, maji na barabara.
Akifafanua zaidi Dkt. Jafo amesema malengo ya Viongozi Wakuu wa Serikali ni kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi inatekelezwa kwa kasi na viwango ili kuwaletea maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla. Kwa upande wao Wajumbe wa kamati hiyo, wameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendesha na kutoa mafunzo ya Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo ambao umeainisha wajibu na nafasi ya Wabunge na Watendaji wa Halmashauri katika kusimamia Mfuko huo.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Ahmed Juma Ngwali aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendesha mafunzo ya Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo mwezi Julai mwaka huu na sasa mafanikio ya mafunzo hayo yameanza kuzaa matunda na kuleta mabadiliko kwa wasimamizi na watendaji wa mfuko huo.
“Tunakushukuru Mhe. Waziri Jafo kwa kufanya ziara Zanzibar mwezi Julai mwaka huu na zaidi ni yale mafunzo yaliyotolewa na Ofisi yako kuhusu Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo kwa sisi Wabunge na Watendaji wa Halmashauri kwa upande wa Zanzibar na PEMBA…Mambo sasa yamebadilika na tunakwenda vizuri” amesema Ngwali.
Aidha Ngwali amesema kabla ya mafunzo hayo, kulikuwa na mkanganyiko kuhusu usimamizi wa fedha hizo jambo lililokuwa likizua malalamiko na lawama kwa watendaji na wasimamizi kuchelewesha fedha katika majimbo na pia na Viongozi kutofahamu taratibu zinazotumika katika ugawaji, utoaji na na upatikanaji wa fedha hizo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Aidha Ngwali aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kupeleka kiasi kikubwa cha fedha za miradi ya maendeleo Zanzibar na kutolea mfano fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Uwanja wa Ndege Pemba na ukarabati wa ujenzi wa barabara ya Wete-ChakeChake ambapo kiasi cha TZS Trilioni 1.4 zimetengwa kutekeleza miradi hiyo.
Nae Mjumbe mwingine wa Kamati hiyo, Mhe. Abdullah Ally Mwinyi ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa juhudi kubwa inazoendelea kuzifanya katika kuendelea kutoa mafunzo usimamizi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo na kueleza kuwa mafunzo hayo yatawezesha kuongeza ufanisi katika usimamizi na uendeshaji wa mfuko huo ambao umekusudia kutekeleza miradi inayoibuliwa na wananchi katika Majimbo.
Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo ulianzishwa kwa Sheria Namba 16 ya mwaka 2009 iliyotungwa na Bunge, ambapo Fedha za Mfuko hutolewa katika Majimbo yote ya uchaguzi Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa kuzingatia vigezo maalum vilivyopitishwa kisheria.