Featured Kitaifa

WHATSAPP YAONGEZA UFANISI KATIKA UPIMAJI WA MAPEMA WA VVU KWA MTOTO ALIYEZALIWA NA MAMA MWENYE MAAMBUKIZI YA UKIMWI(VVU)

Written by mzalendoeditor
Muuguzi katika hospitali ya Nyerere DDH, Nyanchamba Mulaga Musiba akichukua sampuli ya damu kavu kutoka kwa mtoto ambaye mama yake anaishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
 
Imeelezwa kuwa matumizi ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp  yameongeza viwango vya ukaguzi wa ubora wa sampuli ya damu kavu (DBS)  katika hospitali ya wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara (Nyerere DDH) hali inayochangia upatikanaji wa taarifa sahihi za sampuli za damu kavu wakati utambuzi wa awali wa Virusi vya UKIMWI kwa watoto walio chini ya miezi 18 ili kujua hali zao kutokana na wazazi wao kuishi na maambukizi ya VVU.

 
 
Akizungumza Agosti 17,2023 na Waandishi wa Habari waliotembelea Hospitali ya Nyerere ambayo ni hospitali teule ya wilaya ya Serengeti, Muuguzi katika hospitali ya Nyerere DDH, Nyanchamba Mulaga Musiba amesema uanzishwaji wa matumizi ya jukwaa la WhatsApp kama ukaguzi wa ubora wa sampuli za damu kavu ulifikiwa kwa ajili kuboresha sampuli za damu kavu na kuondoa tatizo la sampuli zinazokataliwa maabara(rejected samples).
 
“Mnamo mwaka Mwaka 2021 Mkoa wa Mara uliripotiwa kuwa na kiwango kikubwa cha kutokuwa na sampuli bora za damu kavu katika maabara ya taifa ya upimaji (BMC). Taarifa hizo hazikuwa njema kwetu, lilikuwa ni jambo la kusikitisha kwa programu na kuchukuliwa kama kikwazo katika utoaji wa huduma bora za upimaji na utambuzi wa awali wa VVU kwa watoto chini ya miezi 18 (EID) na jitahada za kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto”,ameeleza .
 
 
Ameeleza kuwa, waliamua kuunda kikundi cha WhatsApp kwa ajili kufuatilia ubora wa ukusanyaji wa sampuli za damu kavu (DBS) katika ngazi ya mkoa huku akiongeza kuwa matumizi ya kundi la WhatsApp kama ukaguzi wa ubora wa sampuli za DBS umefikiwa kwa ajili kuboresha sampuli za damu kavu na kuondoa tatizo ya sampuli zinazokataliwa maabara.

 

Muuguzi katika hospitali ya Nyerere DDH, Nyanchamba Mulaga Musiba

 

 
“Kikundi chetu cha WhatsApp cha mkoa cha damu kavu kina wahusika wakuu wakiwemo wataalamu wa afya katika ngazi ya mkoa na wilaya kama vile maafisa programu, mshauri wa PMTCT, Mratibu wa Afya ya Uzazi wa Mtoto ngazi ya mkoa na waratibu Afya ya Uzazi na wa wilaya kwa kila halmashauri na watoa huduma za afya wanaohusika na ukusanyaji wa sampuli za damu kavu. Pia wataalamu wa maabara ambao ni wazoefu kwenye upimaji wa damu kavu wameunganishwa kwenye jukwaa letu la WhatsApp”,ameeleza.
 
Ameongeza kuwa kupitia kundi hilo la Whatsapp wamekuwa wakibadilishana mawazo, ushauri na kupeana elimu hivyo kufanya mitandao ya kijamii hususani Whatsapp kama njia rahisi ya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Amesema Kikundi hicho kinatumika kama nyenzo shirikishi kutoka kwa kila mtaalamu kuhakikisha kuwa kila sampuli ya mtoto mchanga inakuwa katika ubora unaotakiwa kabla ya mama na mtoto hajaondoka kituoni na kwamba pindi kunapokuwa na wasiwasi wa ubora wa sampuli iliyochukuliwa hupata mrejesho kupitia kikundi cha whatsApp, sampuli ya mtoto mchanga inachukuliwa tena kwa ajili ya kukidhi vigezo vya ubora.
 
“Ninapopata mtoto anatakiwa kuchukuliwa kipimo cha damu kavu katika ngazi ya kituo, kila sampuli ya damu kavu inapochukuliwa moja inatumwa kwenye kikundi cha WhatsApp, hii inaruhusu ukaguzi wa kina wa ubora, huku wataalamu wengi wakitoa maoni kwa wakati mmoja kabla ya mama na mtoto wajaondoka kutoka kituoni kurudi nyumbani.
 
Kama Sampuli ya DBS iko vizuri,namruhusu mama aondoke,kama haijatoka vizuri narudia kumpima mtoto ili kupata majibu sahihi ili kujua hali ya mtoto ambaye mama yake anaishi na maambukizi ya VVU. Haya yote tunataka mtoto asipate maambukizi”, ameeleza Nyanchamba Muuguzi ambaye tangu aanze kufanya kazi Hospitali ya Nyerere DDH miaka 11 sasa hajawahi kupata kesi ya mtoto kupata maambukizi kutoka kwa mama anayeishi na VVU.
 
Amebainisha kuwa Matumizi ya teknolojia kupitia Kundi la Whatsapp yamesaidia kupungua kwa sampuli za damu kavu ambazo hazikidhi vigezo katika maabara ya BMC kutoka sampuli tano (5) kipindi cha Oktoba – Desemba 2021 mpaka sasa kituo hakina sampuli inayorudishwa sababu ya kutokidhi vigezo (zero rejection) wakati wa Q1FY21 hadi sampuli 0 zilizokataliwa wakati wa Q2FY21.
 
 
Katika hatua nyingine amesema kundi hilo la WhatsApp pia limesaidia kuboresha mawasiliano ngazi ya wilaya au Mkoa pamoja na wadau pindi pindi wanapopata changamoto mfano vitenganishi vinapoisha ambapo wamekuwa wakituma tu ujumbe mfupi (SMS) wanaletewa au kupewa majibu na wahusika mara moja.
 
Mratibu Msaidizi wa Afya ya Mama na Mtoto Hospitali ya Nyerere Monica Nyasale amesema tangu mwaka 2018 hadi mwaka huu wamefanikiwa kutoa huduma kwa akina mama 31,000 kati yao 196 walibainika kuwa na maambukizi ya VVU ambao tayari wameanzishiwa huduma ya dawa ili kuwakinga watoto wasipate maambukizi ya VVU.

 

Mratibu Msaidizi wa Afya ya Mama na Mtoto Hospitali ya Nyerere Monica Nyasale
 

 

“Nyerere DDH ni kituo cha matunzo na matibabu ambacho hutoa huduma kamili za VVU. Upimaji wa viwango vya VVU na huduma za kinga kama vile PrEP na usambazaji wa kondomu pia hutolewa kupitia usaidizi wa PEPFAR na CDC na kumekuwa na mipango kadhaa ya utoaji wa huduma bora za utambuzi wa awali wa VVU kwa watoto (EID)”,amesema Nyasale.
 
 
Naye Mtaalamu wa Maabara katika Hospitali ya Nyerere DDH Serengeti, ambayo inatumika kama Hospitali teule ya Wilaya ya Serengeti, Paschal Wamwaro Magayane amesema mbinu hiyo ya kibunifu imekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu hivi sasa wanapata Sampuli zenye ubora na sasa hakuna Sampuli inatakaliwa baada ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa Bugando Mkoani Mwanza.
 
“Kabla ya matumizi ya whatsApp kwenye ukaguzi wa sampuli za damu kavu kituo kilikuwa na changamoto ya kuwafuatilia wa mama ambao sampuli zao zilikataliwa. Hali hii ni tofauti kwa sasa kwa sababu sampuli zisizokidhi vigezo zinarudiwa kabla ya mama kuondoka kituoni. Tunapata sampuli safi tu sasa hivi”, amesema Magayane.

 

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Nyerere DDH Serengeti Dkt. Edgar Saulo Mganyizi
 

 

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Nyerere DDH Serengeti Dkt. Edgar Saulo Mganyizi ameishukuru Serikali ya Marekani na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa wanaotoa kwenye hospitali hiyo iliyoanzishwa mwaka 1980 ikimilikiwa na Kanisa la Mennonite katika ikiwemo kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
 
 
Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa minne inayofadhiliwa na PEPFAR kupitia CDC. Tangu Oktoba 2010, CDC inatoa huduma kamili za VVU ili kufikia udhibiti wa janga la VVU na kufikia lengo la 95-95-95 ifikapo 2030.
 
 
Mpango huu unasaidia Wizara ya Afya (MoH) kufikia lengo la kitaifa la kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) hadi chini ya asilimia nne (<4%) ifikapo mwaka 2026 ikiwa malengo ya programu ni pamoja na kuongeza idadi ya wajawazito na wanaonyonyesha wanaojua hali zao za maambukizi ya VVU, kuongeza idadi ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha walio na VVU wanaopata dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs).
 
Malengo mengine ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matunzo na matibabu kwa akina mama na watoto wachanga wanaoishi na VVU sambamba na kuboresha maisha ya watoto walio zaliwa na mama mwenye VVU na wale watoto tayari wana maambukizi ya VVU..
 
Katika Mkoa wa Mara kuna vituo vya afya 358, ambapo vituo vya afya 107 vinasaidiwa kupitia PEPFAR kutoa huduma za matunzo na matibabu pamoja na kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ( PMTCT).
 
Huduma za utambuzi wa awali wa VVU kwa watoto walio chini ya miezi 18 (EID) hutolewa na wafanyakazi waliofunzwa, na afua muhimu zinasaidiwa ili kuboresha ubora wa huduma za EID, ikiwa ni pamoja na vituo vya kusaidia huduma za EID, usafirishaji wa sampuli za damu kavu (DBS) hadi mahali pa uchunguzi, na urejeshaji wa matokeo ya sampuli kavu (DBS) kwa kutumia mfumo wa barua pepe na kutumia mfumo wa kielektroniki wa rufaa wa sampuli (eSRS).
 
Juhudi hizi zinalenga kutambua watoto walioambukizwa VVU mapema na kuwaunganisha na huduma za dawa za VVU (ART).
Mtaalamu wa Maabara katika Hospitali ya Nyerere DDH Serengeti, Paschal Wamwaro Magayane

About the author

mzalendoeditor