Featured Kitaifa

TUME YA MADINI YAAINISHA MAFANIKIO MAKUBWA

Written by mzalendoeditor

KAIMU Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Agosti 18,2023 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo katika kipindi cha mwaka 2022/2023 na mikakati ya mwaka 2023/2024.

 

SEHEMU ya Waandishi wa habari na Watumishi wa Tume ya Madini wakimsikiliza Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo,akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo katika kipindi cha mwaka 2022/2023 na mikakati ya mwaka 2023/2024.

Na.Alex Sonna-DODOMA

KATIKA kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 masoko na vituo vya ununuzi wa madini vilichangia jumla ya Sh. bilioni 157.4  kama mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini nchini.

Hayo yameelezwa leo Agosti 18,2023 jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo wakati akitoa taarifa  kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo katika kipindi cha mwaka 2022/2023 na mikakati ya mwaka 2023/2024.

Mhandisi Lwamo amesema kuwa, Tume ya Madini imefanikiwa kuanzisha masoko 42 ya madini na vituo vidogo vya kuuzia madini 94 kama mkakati wa kuimarisha udhibiti wa biashara ya madini nchini ili kuongeza mapato yatokanayo na rasilimali madini kwa Serikali.

”Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 masoko na vituo vya ununuzi wa madini vilichangia jumla ya shilingi  bilioni 157.4  kama mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini nchini ikiwa ni sawa na asilimia 23.22 ya makusanyo yote yaliyokusanywa na Tume katika mwaka husika.”amesema Mhandisi Lwamo

Aidha amesema kuwa katika kipindi cha  Mwaka wa Fedha 2022/2023, Tume ya Madini imefanikiwa kutoa jumla ya leseni za uchimbaji madini 9,642 kati ya leseni 9,174 zilizopangwa kutolewa na tume hiyo kwa mwaka wa fedha uliopita.

“Katika kuendelea kuimarisha uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini, Tume imefanikiwa kutoa jumla ya leseni za uchimbaji madini 9,642 ambazo zinajumuisha leseni za uchimbaji mkubwa, uchimbaji wa kati, uchimbaji mdogo, biashara ya madini pamoja na uchenjuaji wa madini, na kati ya leseni zilizotolewa, leseni 6,511 sawa na asilimia 70.97 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo”, alisema Mhandisi Lwamo.

Ameongeza kuwa, kuongezeka kwa utoaji wa leseni hizo unadhihirisha azma ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuongeza mchango wao katika sekta ya Madini.

Amesema kuwa Tume ya Madini  imeendelea kusimamia uwasilishaji wa Mipango ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCPs) kutoka kwa Wamiliki na Waombaji wa leseni za madini pamoja na watoa huduma kama takwa mojawapo la Sheria ya Madini Sura ya 123.

“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23, jumla ya mipango 656 ya Ushirikishwaji wa Watanzania ilipokelewa na kufanyiwa uchambuzi na kati ya mipango iliyowasilishwa, 652 ilikidhi vigezo na kuidhinishwa.” Alimalizia Mhandisi Lwamo.

 Hata hivyo amesema kuwa Mwelekeo wa Sekta ya Madini unalenga  kuhakikisha Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa unafikia asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025 kama inavyofafanuliwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa, Ilani ya  Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 pamoja na Mpango Mkakati wa Tume ya Madini wa Mwaka 2019/2020-2023/2024.

“Katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa, Tume ya Madini inatarajia kuwa na mikakati ifuatayo ili kuwa na shughuli za madini ambazo ni endelevu  za kuimarisha usimamizi na udhibiti katika maeneo ya uzalishaji wa madini ujenzi na madini ya viwandani kwa kuongeza Wakaguzi Wasaidizi wa Madini Ujenzi (AMAs), vitendea kazi (PoS) pamoja na kushirikisha Mamlaka nyingine za Serikali zinazosimamia na kutumia rasilimali hizi yaani Halmashauri, Polisi, TARURA & TANROADS, hii  itasaidia kuuongezeka kwa makusanyo yatokanayo na rasilimali ya madini ujenzi na madini ya viwandani”, amesema Mhandisi Lwamo.

About the author

mzalendoeditor