Featured Kitaifa

TOSCI KUTUMIA SH.BILIONI 12.6 KUTEKELEZA SHUGHULI MBALIMBALI 

Written by mzalendoeditor

Mkurungezi Mkuu wa Taasisi ya kuthibiti ubora wa mbegu Tanzania (TOSCI) Bw.Patrick Ngwediagi,  akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 15,2023 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/24.

Na.Alex Sonna-DODOMA

KATIKA mwaka wa Fedha 2023/24 Taasisi ya kuthibiti ubora wa mbegu Tanzania (TOSCI) inatarajia kutumia kiasi cha Sh.bilioni 12.6 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali.

Hayo yameelezwa leo Agosti 15,2023 jijini Dodoma na Mkurungezi Mkuu wa Taasisi ya kuthibiti ubora wa mbegu Tanzania (TOSCI) Bw.Patrick Ngwediagi, wakati  akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/24.

Bw.Ngwediagi, amesema kuwa  moja ya  shughuli watakayoifanya ni kuendelea na uboreshaji wa shughuli za utafiti na usimamizi wa ubora wa mbegu.

“Taasisi itaendelea kuboresha shughuli za uthibiti na usimamizi wa ubora wa mbegu zilizoanzishwa katika mwaka wa fedha uliopita katika maeneo mbalimbali”amesema Bw.Ngwediagi

Aidha amesema  shughuli nyingine ni kutekeleza mradi wa kuendeleza sekta ya kilimo na uvuvi (AFDB) kwa kujenga maabara yenye uwezo mkubwa.

“Maabara hii itawezesha taasisi kufanya uchambuzi wa mambo mbalimbali yanayohusu mbegu katika makao makuu ya TOSCI”amesema

Hata hivyo amesema kuwa wamepanga kujenga maabara ya mbegu kwenye tawi la taasisi hiyo kanda ya ziwa mkoani Mwanza .

“Pia kuandaa na kutekeleza mkakati wa kuelimisha umma juu ya matumizi ya mbegu zilizothibitishwa ubora za zenye  lebo ya TOSCI.

“Kuthibitisha na kusimamia  ubora wa miche/vipando na pingili za mazao ya miti ya matunda,migomba na miwa”amesema

Aidha amesema katika kipindi cha miaka mitano ilihopita taasisi hiyo imesajili zaidi ya mbegu 647 na kuwachukulia hatua watu wote waliobainika kuuza mbegu feki kwa kuwafikisha mahakamani.

Pia amewataka  wakulima na jamii kwa ujumla kuacha matumizi holela ya mbegu na badala yake watumie ambazo zimethibitishwa ubora ili kuongeza mavuno, tija na kipato.

Amesema ili kilimo kuwa na tija nchini wakulima wanapaswa kutumia mbegu zenye ubora na zilizothibitishwa na taasisi hiyo ili kuongeza mavuno na kipato.

“Wito wangu kwa wakulima na jamii kwa ujumla tumieni mbegu zilizothibitishwa ubora ili kuongeza mavuno,tija na kipato badala ya kuendelea kutumia mbegu ambazo hazina ubora na kupunguza tija kwenye kilimo nchini”amesema

About the author

mzalendoeditor