Featured Kitaifa

RAIS TUCTA ATOA TAMKO SAKATA LA CWT

Written by mzalendoeditor

Rais wa Shirikisho la  Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Tumaini Nyamhokya,akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 12,2023 jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

SAKATA la wanachama wa Chama cha Walimu (CWT) dhidi ya Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu la kupokea na kuridhia kwa asilimia 100 ombi baadhi ya walimu kusitisha malipo ya makato ya ada za chama hicho katika mishara yao limechukua sura mpya.

Akitoa tamko hilo leo Agosti 12,2023 jijini Dodoma Rais wa Shirikisho la  Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Tumaini Nyamhokya, amesema  kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria uliofanywa na kikao cha Baraza hilo la Madiwani wa halmashauri hiyo.

“Leo tarehe 12 Agosti, 2023 TUCTA tumepokea taarifa kupitia wanachama wa CWT halmashauri ya wilaya ya karatu wakionyesha kushangwazawa na tukio la baraza la Madiwani kupokea na kuridhia kwa asilimia 100 ombi la baadhi ya walimu kusitisha malipo ya makato ya ada za chama cha walimu toka katika mishara yao.

“Na badala yake malipo hayo yalipwe Chama walichokitambulisha kwa jina la Chama cha kutetea na kulinda haki za Walimu Tanzania”amesema

Aidha amesema kuwa kitendo hicho cha Baraza la Madiwani siyo tu kimekiuka sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini sura 366 marejeo ya mwaka 2019, pia kimekinzana na utamaduni wa kiugwana na utawala bora wa Mamlaka mbalimbali nchini kutongilia taratibu na kanuni halali za mamlaka nyingine.

“TUCTA tunasema kitendo hiki kinastahili kukemewa kwa nguvu zote kwani sio jambo la kiugwana”amesema

Amesema TUCTA kwa kauli moja wanapinga azimio la Baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Karatu ya kukubali kwa kauli moja na kutekeleza maombi batili ya kusitishwa kwa malipo ya ada za uanachama wa baadhi ya walimu kwa chama cha walimu Tanzania (CWT).

“Kupitia tamko hili TUCTA, tunaiomba serikali isifumbie macho jambo hili,Wizara zenye dhamana ya serikali za Mitaa pamoja na Ofisi ya Waziri mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye ulemavu walikemee jambo hili na kuelekeza Baraza la Madiwani pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri ya Karatu kusitisha mara moja azimio hilo na kuelekeza sheria izingatiwe katika masuala yote yanayohusu haki za wanachama na vyama vya wafanyakazi nchini”amefafanua

Hata hivyo, ameeleza kuwa  kwa mujibu wa taarifa walizozipokea ambazo zimesambaa katika mitandao ya kijami kupitia clip inayoeleza tukio la kikao cha baraza la Madiwani wa Baraza hilo mwenyekiti wa halamshauri hiyo John Mahu alipokea na kuridhia kwa kauli moja maombi hayo.

About the author

mzalendoeditor