Featured Kitaifa

BARAZA LA UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI WATIA FORA NANE NANE 2023, WATOA ZAWADI KWA RAIS SAMIA

Written by mzalendoeditor

Na WMJJWM, Mbeya.

Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi nchini, Fatma Kange amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuwawezesha wanawake hasa kupitia mabazara ya kuwawezesha kiuchumi.

Fatma Kange ametoa shukrani hizo zikiambatana na zawadi mbalimbali kwa Mhe. Dkt. Samia alizozikabidhi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu katika kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya wakulima Agosti 08, 2023.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi zawadi hizo, Fatma ameuomba uongozi wa Wizara kufikisha salaam zao kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan huku wakiahidi kuendelea kumuunga mkono katika juhudi anazozifanya katika kujenga Nchi.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amewashukuru wanawake hao kutokana na kazi zao wanazozifanya lakini uimara wa Jukwaa lao ambalo tayari limeundwa na kuwa na viongozi kwenye ngazi zote.

“Kazi mnayofanya ni kubwa na ya mfano, tutafikisha salaam zenu kwa Mhe.Rais, niwatie shime mzidi kusonga mbele muongeze ubunifu lakini hata teknolojia ikuzeni katika bidhaa zenu” amesema Dkt. Jingu.

Maonesho ya Nane Nane yalioanza Agosti Mosi, 2023 katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, yamefungwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Agosti 08, 2023.

About the author

mzalendoeditor