Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Julai 28,2023 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/2024.
Na.Alex Sonna-DODOMA
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imesema muda wa wananchi wa jiji hilo kupata huduma ya maji utaongezeka kutoka saa 13 hadi 19 mwishoni mwa mwaka 2024.
Hayo ameyasema leo Julai 28.2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/2024.
Amesema kuwa hatua hiyo itakuja baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa miradi ya muda mfupi ya uchimbaji wa visima pembezoni mwa mji.
“Water Service coverage ni asilimia 91, na muda wa utoaji huduma za maji ni saa 13 kwa siku , lengo ni kufikia coverage ya asilimia 93 ifikapo mwaka 2024, hata hihovyo tunaenda kuongeza muda wa utoaji huduma kutoka saa 13 hadi 19 hiyo italeta unafuu kaisi fulani kwa wananchi,”amesema Mhandisi Joseph.
Hata hivyo ameeleza kuwa katika mpango wa muda mfupi,DUWASA inaendelea na utafiti, kuchimba na kuendeleza visima maeneo ya pembezoni mwa mji.
Mhandisi Joseph amesema kuwa lengo la mpango huu ni kupunguza adha kwa wakazi katika maeneo hayo, na kupunguza utegemezi wa chanzo kikubwa cha Mzakwe, wakati tunasubiri uwekezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati jijini Dodoma.
Aidha ameitaja miradi hiyo ni pamoja na wa uboreshaji huduma za majisafi Nzuguni, miradi wa maji Bihawana, mradi wa maji Zuzu-Nala na uchimbaji visima pembezoni mwa mji ili kupata vyanzo vingine vya maji kwa wakazi wa jiji.
Amesema kuwa katika mpango wa muda wa kati, DUWASA kwa kushirikiana na Wizara ya Maji inaendelea kufuatilia hatua mbalimbali za utekelezaji mradi wa Bwawa la Farkwa lililopo wilaya ya Chemba-Dodoma.
Pia amesema kuwa katika mpango wa muda mrefu, DUWASA kwa kushirikiana na wizara inaendelea kufuatilia hatua hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kuja Dodoma.
Mhandisi Joseph amesema kutokana na kuongezeka kwa kasi ya mahitaji ya maji jijini hapa, Mamlaka hiyo inautazama mradi huu kama suluhisho kwa adha ya upatikanaji wa maji.
“Mpango huu unaitwa wa dharura/haraka kwakuwa unawezekana kutekelezwa katika muda mfupi chini ya miaka mitatu na kuweza kuongeza kiasi cha majiji ni Dodoma kwa lita milioni 130 kwa siku,”amesema Mhandisi Joseph.
Hata hivyo amesema kuwa DUWASA inaendelea kuhudumia wakazi wa mjini kwa wastani wa asilimia 20 huku sehemu kubwa inayohudumiwa ni mjini kati na maeneo machache ya pembezoni kama Kikuyu, Area A, Iringa Road na Kizota.
Amesema kwa sasa mji wa Dodoma una wakazi 765,179 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 ambapo takribani asilimia 91 wanapata huduma ya majisafi na salama kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na migao.
Pia amebainisha kuwa tathimini iliyofanyika hivi karibuni ineonesha kuwa mahitaji ya maji mjini ni lita 133,400,000 kwa siku mwaka 2022, lita 146,317,000 kwa siku ifikapo mwaka 2026,lita 204,315,000 kwa siku mwaka 2036 na lita 417,308,000 kwa siku ifikapo mwaka 2051.
Amesema chanzo kuku cha maji kwa matumizi ya wakazi wa mji wa Dodoma ni visima virefu vilivyochimbwa katika bonde la Makutupora eneo la Mzakwe, miundombinu ya uzalishaji maji pamoja na uwezo wa usafirishaji maji ni lita milioni 61.5 kwa siku.
Aidha, kuna vyanzo vingine vidogo kwa maeneo mahsusi ambavyo ni Ihumwa kwa ajili ya Mji wa Serikali, Iyumbu kwa ajili ya Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM), Kata ya Iyumbu, Hospitali ya Benjamini Mkapa na kata ya Nghong’onha ambavyo kwa pamoja vinzalisha lita milioni 5.6 kwa siku.
“Vyanzo vyote hivyo ba vingine vidogo vinafanya uzalishaji wa jumla ya lita milioni 68.6 kwa siku wakati mahitaji ya sasa ni lita milioni 133.4 kwa siku hivyo upungufu huu unaongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na ongezeko la watu na shughuli a kiuchumi na kijamii jijini hapa,”alisema Mhandisi Joseph.
Hata hivyo amesema kuwa Serikali inaendeleza azma yake ya kutoa maji kutoka ziwa Victoria mkoani Mwanza na kuyapeleka Dodoma ili kukabili upungufu uliopo sasa na kukomesha mgao unaoendelea.
“Mipango ya muda mrefu ya kukabiliaana na hali hii ya shida ya maji katika mkoa wa Dodoma ni pamoja na kuleta maji ya ziwa Victoria mkoani Mwanza kuja kutatua kero hii ya ongezeko la mahitaji ya maji ambapo kiasi cha Sh. trioni 1.2 zinahitajika kwa ajili ya mifumo ya kusafirisha maji “alisema Mhandisi Joseph