Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS:WANANCHI JITOKEZENI KUPATA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Philip Mpango amewasihi wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi kupata huduma ya msaada wa kisheria kutoka kwa wataalam wa sheria waliopo katika wilaya na Halmashauri za Mkoa wa Ruvuma.

Mhe. Dk. Mpango ameyasema hayo leo Julai 23 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Nyasa na Mbinga ikiwa ni siku ya Nne ya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi mkoani Ruvuma.

“Jana (Julai 22, 2023) nilizindua rasmi utekelezaji wa Kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Mkoa wa Ruvuma iliyofanyika katika uwanja wa Majimaji, Wilayani Songea. Hivyo nichukue nafasi hii kuwasihi mjitokeze kwa wingi pindi wataalam wa sheria watakapofika katika wilaya zetu,” amesema Makamu wa Rais Dk. Mpango.

Mhe. Dk. Mpango amesema kuwa kampeni hiyo ina lengo la kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kugharamikia wanasheria kuhakikisha wanapata haki zao.

Kwa Upande wake Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Songea Mjini, Mhe. Dk. Damas Ndumbaro amesema kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni mkakati unaotekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wenye lengo la kuongeza uelewa wa sheria na haki za binadamu kwa wananchi wote hususani wanawake,watoto na makundi maalum.

Dkt. Ndumbaro ameongeza kwamba Kampeni hiyo itasaidia kuimarisha huduma za ushauri na msaada wa kisheria hususani kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya pembezoni mwa nchi. Amesema kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia itapita katika kila halmashauri na kila kata, ambapo huduma hizo zitatolewa katika meneo yenye mikusanyiko, vituo vya mabus, vituo vya bodaboda, taasisi mbalimbali kama vile za elimu pamoja na maeneo ya vizuizi ikiwemo mahabusu na magereza.

About the author

mzalendoeditor