Featured Kitaifa

VYUO VYA UALIMU, VETA NA FDC KIINI CHA UTOAJI ELIMU UJUZI

Written by mzalendoeditor

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula amesema Vyuo vya Ualimu, VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vina mchango mkubwa katika mageuzi ya elimu yanayofanyika nchini na kumtaka kila mtumishi kutimiza wajibu wake.

Dkt. Rwezimula amesema hayo Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma alipofanya ziara Chuo cha Ualimu Kasulu kwa lengo la kujitambulisha na kufahamu mazingira ya utendaji ya watumishi katika Chuo hicho.

Amesema kwa sasa Wizara inakaamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na mabadiliko ya mitaala hivyo ili kufanikisha utekelezaji wa Mageuzi hayo taasisi hizo za elimu zinatakiwa kuwa tayari.

“Vyuo vya ualimu ndipo kunazalishwa walimu watakaokwenda kufundisha katika shule zetu hapa nchini na lengo ni kutoa elimu ujuzi hivyo walimu wataandaliwa kwa mlengo huo vilevile kwa VETA na FDC tunategemea kupata wahitimu wenye ujuzi wa kutenda hivyo tunapaswa kuwa tayari,”amesema Dkt. Rwezimula.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia pamoja na masilahi ya watumishi hivyo Wizara itaendelea kuhakikisha mazingira ya utumishi katika taasisi hizi yanaendelea kuboreshwa ili kuleta ufanisi.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ualimu Kasulu Hellen Cheyo ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu kwa kuendelea kuboresha mazingira ya Chuo hicho. Amesema katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2020/21- 2023 Chuo hicho kimepatiwa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.

Ametaja miradi iliyotekelezwa Chuo hapo kuwa ni ujenzi wa ukumbi wa mihadahara kupitia fedha za UVIKO 19, ujenzi wa maktaba, maabara za TEHAMA, Biolojia, Kemia pamoja na ukarabati wa maabara ya biolojia.

About the author

mzalendoeditor