Featured Kitaifa

ZAIDI YA BILIONI MOJA KUENDELEZA UBUNIFU NCHINI

Written by mzalendoeditor

Serikali imetoa zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili ya kuendeleza ubunifu unaozalishwa na wabunifu hapa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati wa kufunga kongamano la nane lililoambatana na maonesho ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Lugano Kusiluka amesema fedha hizo zinalenga kuendeleza miradi 49 ya wabunifu.

Ametaja makundi yatakayonufaika na fedha hizo kuwa ni wabaunifu ambao wanapeleka bunifu zao Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambazo zimefikia hatua ya kubiasharishwa, wanaotokana na MAKISATU na wale wanaotokana na kongano la bunifu (Innovation Cluster).

Pia amesema Wizara inatambua juhudi zinazofanywa na watafiti, wanasayansi, wabunifu na wajasiriamali hivyo itaendelea kuweka mazingira bora ili utafiti na ubunifu viweze kuwa na mchango mkubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi.

“Serikali itaendeleza juhudi za kuboresha na kutekeleza sera ya sayansi, teknolojia kwa lengo la kukuza uelewa na kujenga utamaduni wa kutumia matokeo ya utafiti katika kuboresha sekta ya uzalishai,” alisema.

Prof. Kusiluka amesema maendeleo ya kiuchumi hayawezi kufikiwa bila kuwa na mipango madhubuti, ndio maana serikali imehakikisha shughuli za utafiti na maendeleo zinatengewa fedha .

” Fedha hizi zimekuwa zikitolewa katika taasisi mbalimbali zikiwemo vyuo vikuu, vyuo vya kati, taasisi za utafiti na maendeleo , kwa wabunifu na wajasiriamali wadogo wadogo wanaoratibiwa na Costech,” alisema Prof. Kusiluka.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Dkt. Amos Nungu amesema Tume hiyo imekuwa ikaandaa kongamano hilo ikiwa ni utekelezaji wa jukumu lake la kuishauri Serikali kuhusu masuala yanayohusu Sayansi, Teknolojia na ubunifu

Amesema kongamano hilo limekuwa na mafanikio kutokana na mada zilizowasilishwa na kwamba limehudhuriwa na washiriki 520, zikiwemo taasisi 59 za ndani ya nchi na 5 kitoka nje ya nchi.

“Tumekuwa na maazimio mengi katika kongamano lililokuwa na kauli mbiu iliojielekeza katika mapinduzi ya nne ya viwanda kuwa ni mtambuka, sio tehama peke yake na kupitia kongamano imependekezwa kuwa iundwe kamati itakayomshauri Rais kuhusiana na mapinduzi hayo ya nne ya viwanda “amesema Dkt. Nungu

About the author

mzalendoeditor