Featured Kitaifa

SERIKALI KUANZA UTEKELEZAJI WA HUDUMA ZA AFYA KWA WAZEE WASIOJIWEZA

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wazee pamoja na wananchi wa kata ya Ihumwa, jijini Dodoma katika Maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee yaliyofanyika kimkoa kwenye kata hiyo,leo Juni 15, 2023

Mwenyekiti wa wa Baraza la Ushauri la wazee mkoa wa Dodoma Petro Mpolo akisoma risala ya wazee huo, wakati wa Maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee kimkoa leo Juni 15, 2023 katika kata ya ya ihumwa Jijini Dodoma.

kurugenzi wa Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Subisya Kabuje akitoa salaam za ofisi hiyo kwa wazee, katika maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee Juni 15, 2023, kwenye kata ya Ihumwa jijini Dodoma yalipofanyika kimkoa.

Baadhi ya wazee na wananchi walioshiriki maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee katika mkoa wa Dodoma kwenye kata ya Ihumwa, wakifuatilia matukio yanayoendelea wakati wa maadhimisho hayo Juni 15, 2023.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akimtunuku cheti cha pongezi kwa mchango wake katika jamii mmoja wa wazee wa jiji la Dodoma wakati wa Maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee yaliyofanyika kimkoa kwenye kata ya Ihumwa, leo Juni 15, 2023

Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Wizara ya maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na makundi maalumu imesema inafanya jitihada kushughulikia changamoto za wazee na kuhakikisha suala la huduma za Afya linatekelezwa kwa wazee wasiojiweza kwa kuwasajili na kuwapatia vitambulisho vya matibabu bure (ICHF).

Kwa kudhihirisha hilo kwa kipindi cha Julai, 2022 mpaka Aprili, 2023 Jumla ya Wazee 2,117,637 (Me 1,382,468 na Ke 735,169) wametambuliwa katika Mikoa 26 585,672 (Me 255,496 na Ke 330,176) sawa na asilimia 27.65 walithibitishwa kuwa hawajiwezi na wamepatiwa vitambulisho vya Bima ya Afya kwa ajili ya matibabu.

Waziri mwenye dhamana na Wizara hiyo Dkt.Dorothy Gwajima ameeleza hayo leo June 15,2023 jijini Dodoma kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuelimisha na kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wazee na kueleza kuwa Wizara inaendelea kuhamasisha na kuweka mkazo katika kuelimisha jamii kutambua na kuthamini mchango wa wazee na kuendelea kutekeleza Kampeni ya “MZEE KWANZA” yenye lengo la kumpa kipaumbele mzee katika maeneo yote ya kutolea huduma.

Katika kuboresha huduma za afya kwa wazee amesema jumla ya madirisha 629 ya kutolea huduma za Afya ya Msingi kwa wazee yameanzishwa katika Hospitali za Rufaa, Mikoa, Wilaya na Vituo vya Afya hapa nchini.

“Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 Wazee wanafikia 5,008,339 wanaume 2,232,376 wanawake 2,775,963 ambayo ni sawa na 8.1% ambapo kati ya watanzania wote ni sawa na 61,741,120,kutokana na idadi hii serikali inafanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kundi hili linapata huduma stahiki ili kuboresha Ustawi na Maendeleo yao,”amesema.

Dkt.Gwajima aneyataja maeneo mengine ambayo yanapewa kipaumbele na Serikali kuwa ni huduma ya matunzo kwa Wazee na Wasiojiweza katika Makazi ya Wazee 14 yanayomilikiwa na Serikali yenye wahudumiwa wapatao 259 (Me 157 na Ke 102) kwa kuhakikisha wazee wanapata malazi, mavazi, chakula, huduma za afya, msaada wa kisaikolojia na kijamii pamoja na kuunganishwa na familia zao.

Pamoja na hayo amesema Serikali imendelea kuratibu na kusimamia huduma zinazotolewa na Makazi ya Wazee ya Binafsi 15 yenye wahudumiwa 268(Me 150 na Ke 118) ili kuhakikisha huduma zinazotolewa ni stahiki na kueleza kuwa mabaraza ya Ushauri ya Wazee katika ngazi zote nchini yameundwa na kufikia 20,749 ambapo, Serikali imeendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Mabaraza hayo.

“Ili kuboresha zaidi tumekuwa na utaratibu wa kuwashirikisha Baraza la Taifa katika shughuli mbalimbali za Kiserikali lengo likiwa ni kuhakikisha wazee wanapata sehemu ya kuzungumzia mambo yanayohusu, kuishauri serikali pamoja na kutumia ujuzi wao katika kusaidia mipango ya Serikali,”amesisitiza

Ameeleza kuwa Wizara kwa kushirikiana na Wizara nyingine za Kisekta na Wadau mbalimbali imeendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Mauaji kwa Wazee wa mwaka 2018/2019-2022/23 unaolenga kuhakikisha hakuna mauaji yanayotokea nchini kwa wazee, kuwalinda wazee ili waweze kuishi katika jamii salama na kufurahia uzee wao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma Petro Mpolo amebainisha changamoto zinazowakabili Wazee kuwa zinatokana na mila na desturi potofu, na kueleza kuwa fursa nyingi zinazo wahusu haziwafii kutokana na suala zima la uzee na kuzeeka.

“Kumekuwa na sababu tofauti tofauti zinazosababisha ukatili kwetu ikiwemo mila na desturi zenye kuleta madhara ikiwemo Imani za kishirikina, malezi, umasikini na migogoro ndani ya familia na wanaofanya vitendo hivi ni watu wa karibu na tunao waamini,tumechoka unyanyasaji huu,”amesema

Ameeleza kuwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa mzee huambatana na kuwanyima wazee haki zao za msingi kama chakula, mavazi, kutunzwa, kuheshimiwa na kushirikishwa na kueleza kuwa pamoja na ukatili huo wazee waliowengi wameendelea kutunza upendo wao kwa watoto wao na kuendelea kuitumikia jamíi.

Naye mmoja wa wazee wa Wilaya ya Chamwino Mary Ndahani ametumia siku hiyo kuyanyooshea vidole madawati ya kijinsia kuwa ni kichocheo kikubwa cha migogoro ya familia na kuomba Serikali kuangalia upya mfumo wake kwani unawaumiza wazee.

Amesema mara nyingi wazee wanapopeleka taarifa za ukatili dhidi yao kwenye madawati hayo huwa zinatupiliwa mbali bila kusikilizwa na kuelekezwa kumaliza mazungumzo kifamilia.

“Mzazi akimdhibiti mtoto unaenda kushtakiwa na kuchukuliwa sheria,lakini sisi wazee wao tunapofanyiwa ukatili mnatuelekeza kuyamaliza kifamilia,jambo hili linatuumiza kwa kuwa tunaendelea kuishi Kwenye mateso na kupelekea kufa mapema kwa msongo wa mawazo,”amesema

Kuhusu Malezi ya watoto,Ndahani ameishauri Serikali kuweka udhibiti kwenye maudhui ya vipindi vya runinga ili jamii iwe salama.

Kwa upande wake Katibu wa baraza la wazee Wilaya ya Chamwino Godwin Madeje ameishauri Serikali kuwafikiria Wazee kupata asilimia mbili zilizotengwa kwa ajili yao ili wawe na uhakika wa lishe na afya Bora.

Sambamba na hayo ameiomba Serikali kuingilia kati unyanyasaji wa wazee kwa kutelekezewa wajukuu na kueleza kuwa mtoto anatakiwa kutunzwa na wazazi wake, na hataka kama ikitokea mtoto amebaki kwa babu na bibi yake basi, lazima kuwe na ushirikiano wa karibu na upendo na ufuatiliaji.

“Wazee wanapewa mizigo mizito kulea wajukuu wakati wazazi wao wanakula raha,huu ni ukatili usioelezeka na sisi tunahitaji kutunzwa na tunaomba Serikali kuboresha sheria za kutulinda zenye makali ili tuishi vizuri na kuepukana na ukatili wa aina yoyote ile,”amesisitiza.

About the author

mzalendoeditor