Featured Kitaifa

KATAMBI ABAINISHA MIKAKATI SITA FURSA ZA AJIRA KWA VIJANA

Written by mzalendoeditor

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, imebainisha mikakati sita ya fursa za ajira kwa vijana wanaohitimu.

Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe.Patrobas Katambi ameyasema hayo Juni 13, 2023 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Segerea (CCM), Mhe.Bonnah Kamoli ambaye amehoji serikali imejipangaje kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha vijana wanaohitimu wanapata ajira.

Mhe.Katambi akijibu swali hilo, amesema serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imejipanga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili sekta binafsi iwekeze kwenye sekta zinazoweza kuzalisha fursa nyingi za ajira.

Ametaja mikakati mingine ni kutekeleza programu ya mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa vijana wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo ili kuwezesha vijana husika kuwa na ujuzi unaohitajika na waajiri wa sekta binafsi wa ndani na nje ya nchi.

Pia, amesema serikali inatekeleza Programu ya kuwezesha vijana kushiriki katika Kilimo Biashara (BBTYIA) na Programu ya mafunzo ya vitendo (Atamizi) kwa wahitimu wa fani za uvuvi na ukuzaji viumbe maji.

Kadhalika, amesema mkakati mwingine ni kufanya majadiliano na nchi za kimkakati kwa lengo la kuwezesha kuwa na Hati za Mashirikiano ya Uwili na Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuwezesha wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwatengea maeneo pamoja na kufanya utafiti ili kuwa na uhakika wa kupata madini, kuanzisha vituo 93 na masoko 42 ya kuuzia madini.

About the author

mzalendoeditor