Featured Kitaifa

RAIS MSTAAFU DKT.KIKWETE ATETA  NA KAMISHNA WA UMOJA WA ULAYA  (EU)

Written by mzalendoeditor

Rais Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Ubia wa Elimu Duniani (GPE) Dkt. Jakaya Kikwete amekutana na Bi. Jutta Urpilainen, Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa kwa lengo la kujadili ushirikiano zaidi kati ya EU na GPE. Mkutano huo uliofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya yaliyopo Brussels, Ubelgiji ulihudhuriwa pia na Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE, Bi. Laura Fringeti na Mawaziri wa Elimu kutoka katika nchi walikutana na Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Jutta Urpilainen. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Mawaziri wa Elimu kutoka nchi ambazo zinafadhiliwa na GPE katika kutekeleza miradi mbalimbali ya elimu.

Pamoja na mambo mengine katika Mkutano huo Kamishna Jutta Urpilainen alimuhakikishia Mwenyekiti wa Bodi na wajumbe alioambatana nao kuwa EU inatambua na kuthamini kazi kubwa inayoendelea kufanywa na GPE katika kusaidia upatikanaji wa elimu ya msingi kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu hususan kutoka katika nchi zinazoendelea na zile zinazoathiriwa na changamoto za ulinzi na usalama na mbadiliko ya tabia nchi.

Aidha, Kamishna huyo alitumia fursa ya kukutana na ujumbe huo kutangaza kuwa Umoja wa Ulaya umefanya uamuzi wa kuongeza kiasi cha fedha kinachotolewa na EU kwa GPE kutoka asilimia 7 hadi 13. Umoja wa Ulaya ndiyo mchangiaji mkubwa zaidi wa bajeti ya GPE ikichangia zaidi ya asilimia 50 ya bajeti ya Taasisi hiyo.

Tanzania ni moja ya nchi zinazonufaika na miradi inayotekelezwa na GPE ambapo mwaka 2020 ilipokea msaada wa Dola za Marekani milioni 112 kusaidia jitihada za Serikali kuboresha elimu ya msingi nchini kwa kuhakikisha watoto wote wanapata elimu ya msingi, hususan watoto wa kike na wale wanaotoka kwenye mazingira magumu.

About the author

mzalendoeditor