Tazama Video Operesheni Tokomeza Bangi Arusha ambapo Magunia 931 yamekamatwa, Hekari 953 zimeteketezwa na watuhumiwa 16 wamekamatwa
Na Mwandishi wetu – Arusha
Kufuatilia operesheni maalumu ya tokomeza bangi mkoani Arusha iliyoendeshwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa muda wa siku nane jumla ya magunia 931 ya bangi kavu iliyokuwa tayari kuingizwa sokoni yamekamatwa na hekari 953 za mashamba ya bangi yanayokadiriwa kuwa na magunia 4765 ya bangi mbichi yameharibiwa/yameteketezwa.
Akizungumzia kuhusu Operesheni hiyo ya kukamata, kuharibu na kuteketeza dawa za kulevya iliyofanyika kuanzia Mei 31,2023 hadi Juni 7, 2023 katika wilaya ya Arumeru, Arusha Jiji na Monduli, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo amesema pia watuhumiwa 16 walikamatwa kuhusiana na matukio hayo.
“Operesheni maalumu ya tokomeza bangi mkoani Arusha imefanyika kwa muda wa siku nane katika wilaya ya Arumeru, Arusha Jiji na Monduli ambapo jumla ya gunia 931 za bangi kavu iliyokuwa tayari kuingizwa sokoni ilikamatwa. Pia hekari 953 zinazokadiriwa kuwa na gunia 4765 za bangi mbichi (makadirio ya gunia tano kila hekari) ziliteketezwa na watuhumiwa 16 walikamatwa”,ameeleza Lyimo.
Ameongeza kuwa katika Operesheni hiyo pia dawa za kulevya aina ya heroine kete 2716 zilikamatwa.
Ameeleza kuwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo yote nchini ili kuhakikisha kilimo cha bangi na mirungi kinatokomezwa kabisa na wananchi kujikita katika kilimo cha mazao mbadala ya biashara na chakula.
Operesheni hiyo imefanyika kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kufanya operesheni nchi nzima ili kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa nchini.
Operesheni hiyo pia ilianza kufanyika siku moja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) kutoa taarifa ya hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa mwaka 2022 ambayo iliitaja mikoa ya Arusha, Iringa, Morogoro na Manyara kujihusisha na kilimo cha bangi kwa kiasi kikubwa.