Asila Twaha, Songwe
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bw. Sospeter Mtwale amewataka Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kutoa elimu kwa wananchi na kushirikiana kutatua kero zao.
Mtwale ameyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo viongozi wa Halmashauri, Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wa Mkoa wa Songwe lengo ni kuongeza uwezo na ufanisi kutekeleza majukumu yao.
“mafunzo haya sio tu kwa Mkoa wa Songwe bali yatafanyika nchi nzima ili kuwaongezea uwezo wa kutekeleza majukumu yenu na kuwa karibu na wananchi sababu mambo mengi yanaanzia kwenu” Mtwale
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi kwa watumishi na ilishatoa vitendea kazi kama pikipiki kwa Maafisa Tarafa kwa ajili kurahisisha shughuli za kiutendaji hasa kusikiliza kero na changamoto za wananchi.
“msisubiri mpaka viongozi wakubwa wafike kwa wananchi ndio watatue kero kafuatilieni na kuhimiza utekelezaji wa Sera za Serikali kila mtu katika eneo lake na kuhakikisha kuwa zinatekelezwa ipasavyo kwa kutenda haki na kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu”
Mtwale amesema, uzoefu unaonesha kuwepo kwa changamoto zinazoathiri utoaji wa huduma kwa wananchi katika ngazi ya Kata,Tarafa na Halmashauri zinazotokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika utendaji kazi wa kila siku.
Amefafanua changamoto hizo ni pamoja na kuwepo kwa migogoro ya kiutendaji kati ya wataalam na viongozi na wataalam wengine katika ngazi hizo, ufuatiliaji na usimamizi usioridhisha wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye ngazi za msingi, kutotatuliwa kwa wakati kero za wananchi na wadau wengine katika ngazi za msingi na kutokuwa na uelewa katika baadhi ya Sera, Sheria na Miongozo inayotakiwa kusimamiwa na kuitekeleza.
Amesema Mtendaji Mkuu wa Kata ni kiungo cha uongozi kwa Idara zote kwenye Kata hivyo, anatakiwa kushiriki, kutoa ushauri kuhusu upangaji wa mipango ya maendeleo katika eneo lake lakini pia kusimamia upangaji wa Mipango Shirikishi ya Maendeleo ya Kata na kupokea na kutatua matatizo na malalamiko ya wananchi katika kata.
Kwa upande wa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Bi. Happiness Seneda ameshukuru uongozi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kuandaa mafunzo kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata amesema wataalam hao ndio watendaji wa moja kwa moja kwa wananchi.
Naye Afisa Tarafa Kamsamba Halmashauri ya Wilaya ya Momba Bw. Haji Ibrahim ameishukuru Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kuandaa mfunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo amesema kama mtumishi wa umma akijengewa uwezo inasaidia kufanya kazi zake kwa ufanisi lakini matarajio yaliyokusudiwa na Serikali kuyatimiza.
Aidha amesema, kunautofauti ya mtu aliyejengewa uwezo katika mafunzo na asiyejengewa uwezo, katika mafunzo hayo kupitia mada tutakazofundishwa itatusaidia kuongeza ufanisi katika majukumu yetu na kubadilika kwa kutumia mbinu tulizofundishwa kusikiliza na kutatua kero na changamoto za wananchi katika kazi.