Featured Michezo

RAIS SAMIA AWATAKA WATANZANIA KUWA WAZALENDO KATIKA MICHEZO

Written by mzalendoeditor

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Wachezaji na Makocha wa timu ya Yanga wakati wa hafla ya kuwapongeza kwa kufanikiwa kufika na kucheza mchezo wa Fainali ya Mashindano ya Shirikisho Afrika (CAF) nchini Algeria. Hafla hiyo ya kuwapongeza Yanga imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 05 June, 2023.

………..

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania na mashabiki wa michezo kuweka mbele uzalendo katika michezo kwa maslahi ya taifa.

Rais Samia amesema hayo wakati wa hafla ya chakula cha usiku ya kuipongeza Timu ya Yanga kwa hatua waliyofikia ya kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) iliyofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Ikulu.

Aidha, Rais Samia amesema timu yoyote itakayowakilisha Tanzania katika mashindano ya michezo ya kimataifa ichukuliwe kama timu ya taifa na utani wa jadi ufanyike katika mechi za nyumbani pekee.

Vile vile, Rais Samia amesema hatua ya Timu ya Yanga kufika kwenye mashindano ya CAF imeleta heshima na kurejesha nchi katika ramani ya kisoka na michezo kwa ujumla.

Hali kadhalika, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kufanya jitihada katika michezo ili kuiwezesha nchi kukaa kwenye ramani ya michezo duniani.

Rais Samia pia amewapongeza wapenzi na mashabiki wa Timu ya Yanga kwa hamasa waliyokuwa wakiitoa kwa wachezaji wa Yanga wakati wa mashindano hayo.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ametoa wito kwa Serikali za Mitaa nchini kuweka mkazo katika michezo kwa kuwa na viwanja katika maeneo yao.  

About the author

mzalendoeditor