Featured Kitaifa

MTAA WA MWAJA,KATA YA CHAMWINO KINARA USAFI WA MAZINGIRA DODOMA

Written by mzalendoeditor

Na. Dennis Gondwe, CHAMWINO

MTAA wa Mwaja uliyopo Kata ya Chamwino umepongezwa kwa juhudi zake za usafi wa mazingira na kupewa cheti na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuthamini juhudi hizo.

Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa kata ya Chamwino, Jumanne Ngede alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi waliojitokeza kushiriki usafi wa mazingira katika Mtaa wa Mwaja uliopo Kata ya Chamwino jijini Dodoma.

Ngede alisema kuwa amefurahishwa na muitikio mkubwa wa wananchi katika zoezi la usafi wa siku ya Jumamosi. “Mtaa wa Mwaja umeingia katika rekodi ya mtaa msafi katika mazingira kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Hongera sana, lakini msirudi nyuma katika suala la usafi. Tuendelee kuhimizana kufanya usafi wa mazingira. Wananchi wote tunafahamu kuwa kufanya usafi ni kwamujibu wa sheria, lakini kwa wakazi wa Mwaja usafi ni jadi yetu” alisema Ngede.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Usafi na usimamizi wa taka katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alimtaja Diwani huyo kuwa wa mfano katika kusimamia usafi wa mazingira. “Niwapongeze sana mnavyodumisha usafi kila Jumamosi ili kuhakikisha mazingira ya mitaa na kata yanakuwa safi. Mazingira safi yanatuepusha na magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu. Mtakumbuka tangu tumeanza kutekeleza kampeni ya usafi, ugonjwa wa kipindupindu umekuwa historia katika Jiji la Dodoma” alisema Kimaro.

Akiongelea maeneo yaliyosanyiwa usafi katika zoezi hilo, alisema kuwa usafi umefanyika katika maeneo mbalimbali ya Mtaa wa Mwaja. “Miongoni mwa maeneo yaliyofanywa usafi wa pamoja ni eneo la makaburi ya Hijra. Niwapongeze kwa mara nyingine wote mlioshiriki zoezi la usafi katika makaburi haya. Imani yangu kufanya usafi katika eneo walipolala wenzetu waliotangulia ni sehemu ya ibada kwa sisi tulio hai” alisema Kimaro.

Ikumbukwe kuwa tarehe 11 Mei, 2023 Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma lilitoa pongezi na vyeti kwa mitaa minne iliyofanya vizuri katika ushiriki wa viongozi na wananchi katika usafi wa mazingira Mtaa wa Mwaja kutoka Kata ya Chamwino ukiwa miongoni kwa kipindi cha robo ya tatu (Januari-Machi), 2023.

About the author

mzalendoeditor