Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses Kusiluka amezitaka Kamati za Ushauri wa Kisekta za Vyuo kutoa mapendekezo yatakayosaidia Vyuo kutatua changamaoto za ajira huku zikishauri kuhusu mahitaji ya soko la ajira.
Dkt. Kusiluka ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam akizindua Kamati ya Ushauri ya Kisekta ya Chuo Kikuu Ardhi ambapo amesema kwa kufanya hivyo zitakuwa zimetekeleza jukumu pia la kuwa kiunganishi kati ya jamii na vyuo.
“Kamati mna jukumu kubwa la kuhakikisha kazi za vyuo na Mradi zinakwenda, niombe iandaliwe miongozo ili hata baada ya mradi kuisha kamati hizi ziendelee kufanye kazi,” amesema Dkt. Kusiluka.
Akizungumzia utekelezaji wa Mradi wa HEET amevitaka Vyuo na Taasisi zilizopatiwa fedha za utekelezaji wa Mradi huo kutumia fedha hizo kama zilivyopangwa ili malengo ya Mradi yaweze kutimia.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amezitaka Taasisi za Elimu ya Juu kutumia Kamati za Ushauri za Kisekta kufanya tathmini ya mara kwa mara na kupima namna ambavyo huduma zitolewazo zinanufaisha jamii na kuisaidia Serikali katika kujenga uchumi imara.
“Uanzishwaji wa Kamati hizi pamoja na mambo mengine unalenga kusaidia kuboresha uwezo wa Vyuo kuandaa mitaala, kufanya tafiti na kutoa huduma za jamii zinazoendana na mahitaji ya soko hivyo zitumieni vizuri,”amesema Prof. Nombo.
Akizungumzia Mradi wa HEET Prof. Nombo amesema Serikali ilivyobuni na kuanza kutekeleza Mradi wa HEET kwenye taasisi za Elimu ya Juu chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia ililenga kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kujenga miundombinu mipya na kukarabati iliyopo.
Prof. Nombo ametaja malengo mengine ya Mradi kuwa ni pamoja na kusomesha wanataaluma katika ngazi ya shahadaza umahiri na za uzamivu katika fani za kipaumbele, Kuboresha mifumo ya kitaasisi katika elimu ya juu kuimarisha matumizi ya Tehama katika ufundishaji na ujifunzaji, kuandaa mitaala mipya na kuhuisha iliyopo ili iendane na soko la ajira.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Ardhi Prof. Evaristo Liwa amesema Kamati teule wanatoka katika Taasisi ambazo majukumu yake yanaendana na fani zinazofundishwa Chuo Kikuu Ardhi.
Ametaja wajumbe wa Kamati teule kuwa ni Bw. Hamad Abdalla Mkurugenzi Mkuu NHC, Dkt. Matiko Mturi Mkurugenzi Mkuu Baraza la Taifa la Ujenzi, Bw. Nathaniel Nhonge Kamishna wa Ardhi, Prof. Evaristo Liwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Prof. John Lupala Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Prof. Ally Namangaya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango fedha na Utawala Ardhi, Elirehema Kaaya Katibu Mkuu ALAT.
Ametaja wengine kuwa ni Mhandisi Mbogo Futakamba Mwenyekiti Jukwaa la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika usimamizi na uendelezaji wa Rasilimaliza Maji, Dkt. Donald Mmari Mkurugenzi Mtendaji REPOA, Bw Innocent Alex raisi wa Serikali ya Wanafunzi (ARUSO) Ardhi, Alfred Luanda Mstaafu wa Chuo Kikuu ARDHI, Dkt. Samweli Mafwenga Mkurugenzi Mkuu NEMC, Alphayo Kidata Kamishna Generali TRA, Husein Ally Mkurugenzi Mahusiano Kampuni ya Bakhresa, na Mhandisi Geofrey Mtimbange Mining Meneja Kiwanda cha Sement Twiga.
Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses Kusiluka,akizungumza wakati akizindua Kamati ya Ushauri ya Kisekta ya Chuo Kikuu Ardhi leo Mei 26,2023 jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo,,akizungumza wakati wa uzinduzi Kamati ya Ushauri ya Kisekta ya Chuo Kikuu Ardhi leo Mei 26,2023 jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses Kusiluka (hayupo pichani) wakati akizindua Kamati ya Ushauri ya Kisekta ya Chuo Kikuu Ardhi leo Mei 26,2023 jijini Dar es Salaam.