Featured Kitaifa

WAZIRI UMMY AITAKA JAMII KUACHA MILA NA DESTURI POTOFU JUU YA MASUALA YA HEDHI 

Written by mzalendoeditor

 
Na. WAF – Dodoma
 
Wito umetolewa kwa jamii kuwa na uelewa kuwa hedhi sio balaa, ugonjwa wala sio laana bali ni mabadiliko ya hali ya kawaida yanayomtokea mwanamke au msichana mara baada ya kubalehe kama ishara kwenye mfumo wa maumbile yake ya uzazi.
 
Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwenye maadhimisho ya wiki ya hedhi salama Duniani yaliyofanyika katika Shule ya Wasichana Bunge Sekondari, Dodoma.
 
“Suala la hedhi limekuwa likionekana ni kama uchafu, usiri, nataka niwaambie kuwa hedhi siyo ugonjwa, balaa wala laana, kwa kuwa tayari ni mwanamke haya ni mabadiliko ya kawaida na jambo hili ni la kawaida na tupaze sauti kujenga uelewa wa jamii kuhusu masuala ya hedhi salama” amesema Waziri Ummy huku kuitaka jamii kuchukua hatua kuachana na mila, desturi na imani potofu juu ya masuala ya hedhi ili kuweza kuwasaidia wanawake na wasichana kuondokana na kunyanyapaliwa na kutengwa kutokana na hali ambayo Mwenyezi Mungu amewaumba nayo.
 
Amesema maana ya hedhi salama ni hali ya msichana au mwanamke kuwa kwenye mazingira salama wakati wa mzunguko wake wa hedhi na anapata huduma zote muhimu ikiwemo miundombinu ya vyoo vyenye usiri, maji safi, taulo za kike, utupaji salama wa vifaa au taulo za kike zilizotumika pamoja na uelewa sahihi juu ya hedhi na mabadiliko ya mwili.
 
“Hedhi isiyo salama inaweza kuchangiwa na miundombinu duni ya vyoo, kukosekana kwa maji safi na salama, matumizi ya vifaa vya hedhi visivyo salama, utupaji ovyo wa vifaa vilivyotumika na uelewa duni juu ya hedhi.” Amesema Waziri Ummy.
 
“Takwimu zinaonyesha kuwa nchini Tanzania wanawake Milioni 13,750,122 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 hupata hedhi kila Mwaka. Idadi hii ni kubwa na hivyo jamii ina kila sababu ya kuhakikisha kuwa kundi hilo linapata huduma bora wakati wa hedhi ikiwemo kuhakikisha uwepo wa maji, sabuni na taulo za kike ili kufanya hedhi iwe salama kwao.” Amesema Waziri Ummy
 
Hata hivyo, Waziri Ummy amesema utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) pamoja na OR -TAMISEMI kwa kushirikiana na Wadau wa Hedhi Salama mwaka 2021, yanaonesha kuwepo kwa changamoto katika ngazi ya jamii hususan uelewa mdogo juu ya hedhi salama kwa wasichana ambapo wenye uelewa ni asilimia 28 tu.
 
“Kuna haja ya kila sekta nchini kuhakikisha tunaungana kwa pamoja kuimarisha afya ya hedhi kwa wasichana na wanawake kwa ujumla ili wasikwame katika kushiriki kwenye maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla.
 
“Napenda kuwasisitiza kuwa, tutumie maadhimisho ya mwaka huu kuhamasisha na kuwakumbusha Watanzania, Viongozi wa Serikali na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kutambua kuwa hedhi salama ni muhimu kwa afya, tuvunje ukimya kwa kuelimisha jamii kuachana na mila na desturi potofu kuhusu hedhi.“ Amesema Waziri Ummy.

About the author

mzalendoeditor