Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO KATIKA MKUTANO WA MWAKA WA AfDB – MISRI.

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati wa majadiliano ya Viongozi wa Juu kuhusu kuhusu kuboresha  utaratibu wa ufadhili wa miradi ya maendeleo na majukumu ya taasisi za fedha  yaliofanyika katika  Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Sharm El Sheikh nchini Misri leo tarehe Mei 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema upo umuhimu wa kuboresha utaratibu wa ufadhili wa miradi ya maendeleo na majukumu ya taasisi za fedha za kimataifa ili kuendana na mabadiliko yaliotokea duniani tangu kuundwa kwa taasisi hizo.

Makamu wa Rais amesema hayo katika majadiliano ya viongozi wa ngazi ya juu katika mjadala uliohusu “kuboresha  utaratibu wa ufadhili wa miradi ya maendeleo na majukumu ya taasisi za fedha za kimataifa” yaliofanyika katika Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Sharm El Sheikh nchini Misri.

Amesema taasisi za fedha za kimataifa ziliundwa kipindi ambacho ni tofauti na sasa ambapo dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali mpya kama vile mabadiliko ya tabianchi, majanga mbalimbali ya asili, maradhi ya mlipuko, uhaba wa chakula pamoja na migogoro ya kimataifa na vita.

Aidha amesema kuongezeka kwa idadi ya watu duniani hususani kwa bara la Afrika lazima kuzingatiwa katika maboresho ya taasisi za kimataifa za fedha kwani bado uwakilishi wa Afrika katika taasisi hizo hauendani na idadi ya watu waliopo barani humo.

Makamu wa Rais amesema ni vema katika maboresho ya taasisi za kimataifa za fedha kuweka utaratibu wa kuzingatia vipaumbele vya mataifa husika wakati wa utoaji wa ufadhili pamoja na kuweka mkazo katika malengo ya maendeleo endelevu.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema inapaswa kupitiwa upya masharti magumu na mchakato mrefu katika utoaji wa fedha za maendeleo pamoja na kutoa wito kwa taasisi hizo kuongeza mtaji kutoka vyanzo mbalimbali ili kuweza kuendana na uhitaji wa nchi zinazoendelea. Pia amesema ipo haja kupunguza michakato ya upataji fedha kutoka katika taasisi hizo pamoja na kuunga mkono miradi ilianzishwa na wawekezaji wa ndani wa sekta binafsi.

Mkutano huo umehudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali wakiongozwa na Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi, Taasisi za Kimataifa, Mawaziri wa Fedha na Magavana, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi, Mashirika ya Kimataifa, Benki ya Maendeleo ya Afrika ikiongozwa na Rais wa Benki hiyo Dkt. Akinumwi Adesina, Viongozi kutoka Umoja wa Afrika pamoja na wadau mbalimbali wa fedha na mazingira.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Misri Mheshimiwa Mostafa Madbouly, mazungumzo yaliofanyika katika kituo cha mikutano cha Sharm El Sheikh nchini Misri. Katika mazungumzo hayo masuala mbalimbali ya ushirikiano yamejadiliwa ikiwemo nishati na mazingira.

Vilevile Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mteule wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (Cop 28) Dkt. Sultan bin Ahmed Al Jaber ambaye pia ni mjumbe maalum wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Mazungumzo hayo yamefanyika katika kituo cha mikutano cha Sharm El Sheikh nchini Misri yaliojikita katika masuala mbalimbali ya ushirikiano wa uhifadhi wa mazingira.

Makamu wa Rais yupo nchini Misri kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika katika mji wa Sharm El Sheikh.

About the author

mzalendoeditor