Featured Kitaifa

HAKUNA HAKI BILA UWAJIBIKAJI KATIKA UTUMISHI WA UMMA

Written by mzalendoeditor

 

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo akifungua mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuhusu sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma. Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Cha Uongozi wa Mwalimu Nyerere Kibaha mkoani Pwani.

 Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Bw. James Kibamba, akimkaribisha Bi. Saraha Mwaipopo, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali (hayupo pichani) kufungua mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya wa Ofisi hiyo kuhusu sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma yaliyofanyika Kibaha

Waajiriwa wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakimsikiliza kwa makini Bi. Sarah Mwaipopo, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo elekezi kuhusu sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma yaliyofanyika Kibaha Mkoani Pwani.

Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakimsikiliza kwa makini Bi. Sarah Mwaipopo, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya (hawapo pichani) wa Ofisi hiyo yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani.

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sarah Mwaipopo akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha kwa ajil ya kufungua mafunzo elekezi ya siku mbili kwa waajiriwa wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sarah Mwaipopo (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na waajiriwa wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali baada ya kufungua mafuzo elekezi kwa watumishi hao yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani. Wa pili kulia Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, James Kibamba wa Ofisi hiyo.

Watumishi wapya kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu Mkuu wa Serikali wametakiwa kuwajibika ipasavyo katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi kwa kuwa hakuna haki bila uwajibikaji katika Utumishi wa Umma.

Hayo yamesemwa leo tarehe 4 Mei, 2023 na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo wakati akifungua mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) yenye lengo la kuwajengea uwezo kuhusu masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwemo kufanyakazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.

Akizungumzia aina ya mafunzo yatakayotolewa, Bi. Mwaipopo amesema kuwa Ofisi hiyo imekusudia kuwajengea uwezo watumishi hao katika masuala mbalimbali yanayohusu majukumu yao, haki na wajibu wao kama watumishi wa umma, Muundo wa Serikali, taratibu za utendaji kazi, maadili, nidhamu, uadilifu na ustahimilivu ambavyo vyote kwa pamoja vinapaswa kuzingatiwa ili kuimarisha utendaji kazi kwa watumishi wa umma hususan kwa ajira mpya.

Ameleza kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa matakwa ya kisheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ambpo Ofisi imeona umuhimu wa kutenga bajeti ili kufanikisha mafunzo haya muhimu yatakayowajenga na kuwapa uelewa katika masuala mbalimbali ya kiutumishi.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Bi. Mwaipopo amewaleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia katika kuimarisha utendaji kazi, nidhamu na maadili ikiwa ni pamoja kuwawezesha kuepuka makosa mbalimbali ya kinidhamu na yale ya kiutumishi ambayo yangeweza kufanyika kwa kukosa uelewa ili kuweza kuyaepuka wakiwa mahali pa kazi.

Aidha, amewataka watumishi wapya kujifunza na kuelewa vyema dira, dhima na misingi muhimu ambayo Taasisi imejiwekea katika utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya usimamizi wa mashauri ya madai na usuluhishi yanayofunguliwa na au dhidi ya Serikali, ndani na nje ya nchi.

Misingi hiyo inahusu uwajibikaji, uadilifu, uaminifu na weledi ambayo ikitekelezwa vyema ni nguzo ya maendeleo endelevu ya nchi yetu.

Naye Francis Oswald, Wakili wa Serikali ameishukuru Ofisi kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu ambayo yatawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamewahusisha watumishi 64 waajiriwa wapya wa Ofisi hiyo wa kada mbali mbali ikiwemo Mawakili wa Serikali 41, Maafisa TEHAMA 2, Makatibu sheria 4, Katibu Muhtasi 3, madereva 9, Watunza Kumbukumbu 4 na Afisa Usafirishaji mmoja.

About the author

mzalendoeditor