Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akielezea kitakwimu hali ya vifo vya watoto chini ya miaka Mitano vimepungua pamoja na ufikaji wa cliniki kwa wajawazito
Na. Catherine Sungura-Dodoma.
Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu amewataka akina mama wajawazito wanaofika kwenye Kliniki za Uzazi, Mama na Mto kupimwa wingi wa damu, mkojo kuangalia wingi wa protini, shinikizo la damu pamoja na kusikiliza mapigo ya moyo ya mtoto bila kutozwa gharama zozote.
Haya ameyasema leo wakati wa kukabidhi vifaa tiba vya kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kwa vituo ishirini vya halmashauri za Mkoa wa Dodoma vyenye thamani ya Shilingi milioni 45 .
Waziri Ummy amesema kuwa vipimo hivyo ni muhimu kwa wajawazito ili kuweza kuepusha kifafa cha mimba na vifo kwa wajawazito.
“Ili kuweza kumuokoa mama mjamzito anapofika kliniki ni vyema kupimwa vipimo hivyo muhimu, vipimo hivi vyote ni bure na ni lazima viwepo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vyote nchini.
Aidha, waziri Ummy amesema Serikali itahakikisha upatikanaji wa 100% wa dawa za kuzuia kutoka damu wakati wa kujifungua, dawa za kuongeza damu na dawa za kuzuia kifafa cha mimba katika vituo vya afya vya umma nchini.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatimiza wajibu wake kwa kujenga majengo,kuboresha miundombinu, kuongeza ajira pamoja na kununua vifaa tiba , hivi sasa tunapata fedha za dawa kila mwezi shilingi bilioni 20, tutahakikisha hizi dawa tatu zitapatika kwa asilimia 100”. Amesema Mhe. Ummy
Hata hivyo Waziri Ummy amezitaka Timu za afya za uendeshaji za Halmashauri nchini kufanya usimamizi shirikishi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuwajengea uwezo watoa huduma za afya, “Huu ndio muelekeo wa wizara, twende kwenye masuala ya kuwawezesha wataalamu wetu kwenye vituo vya afya na kuona kipi kinafanyika tunaweza kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga kama tutaongeza kutoa huduma bora za afya”. Alisisitiza.
Akitaja taarifa za Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya na Utafiti wa Kiashiria cha Malaria (DHS/MIS) ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa nchi imepiga hatua katika viashiria vingi vya afya vya mama na mtoto mathalani vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimeshuka kutoka 67 kati ya vizazi hai 1000 mwaka 2015/2016 hadi 43 kwa kila vizazi hai 100.
“Mahudhurio kliniki ya wajawazito mara nne na zaidi kutoka 53% hadi 65%, aidha, wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya huduma wameongezeka kutoka 63% hadi 81% na wanaojifungua chini ya uangalizi wa mtoa huduma mwenye ujuzi kutoka 66% hadi 85%”.
Waziri Ummy hakusita kuwapongeza Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kubuni mradi huo kwani utasaidia harakati za Serikali za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuwapa kipaumbele kwenye huduma za mama na mtoto.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy amewasisitiza watoa huduma za afya kote nchini kuzingatia taaluma, weledi , maadili na viapo vyao vya utumishi wa afya ili kuokoa maisha ya watu wanaofika kupata huduma kwenye vituo vyao.
Naye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Lugano Kusiluka amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kazi kubwa anayofanya katika kuimarisha huduma za afya ikiwemo huduma za mama na mtoto kwa kuwekezaji mkubwa wa miundombinu, vifaa tiba na ajira katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Amesema UDOM wanao mpango mkakati wa miaka mitano kwa lengo la kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali ikiwemo afya ya jamii hivyo wanayo sababu ya kuonesha uwekezaji wa chuo kikuu hicho kinaleta tija kwa upande wa mradi huo lengo ni kuongeza na kuboresha huduma jumuishi ya Kifua Kikuu (TB), UKIMWI na Malaria kabla na baada ya kujifungua ili kumuheshimisha mama.
Mradi jumuishi wa TB, UKIMWI na Malaria ni mradi wa miaka miwili unafadhiliwa na Mfuko wa Global Fundi na Liverpoolof Tropic of Medicine kwa kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya lengo likiwa ni kuboresha huduma za afya ya mama kabla, wakati na baada ya kujifungua ili kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi .