LICHA ya kutoka sare ya bila kufunga Timu ya Yanga SC imeandika historia Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa mara ya kwanza imetinga hatua ya Nusu Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kutoka sare ya kutofungana na Rivers United kutoka nchini Nigeria mchezo uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Yanga imepata nafasi hiyo baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Nigeria.
Baada ya Simba SC kushindwa kutinga nusu Fainali ya klabu bingwa Afrika kwa kuondoshwa na Wydad Casablanca kwa mikwaju ya Penalti 4-3 Sasa Tanzania imeingiza timu moja nusu Fainali ya Michuano hiyo.
Sasa rasmi Yanga SC itakutana na Marumo Gallants kutoka Afrika Kusini waliwatoa Pyramids ya Misri kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya leo kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Mchezo wa kwanza wa nusu Fainali unatarajia kuchezwa Mei 14 au 15 mwaka huu uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kabla ya wiki moja marudiano kuchezwa nchini Afrika Kusini.
Timu nyingine ambayo imefuzu hiyo ni ASEC Mimosas ya Ivory Coastal baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya US Monastir sasa inamsubiri Mshindi kati ya FAR Rabat ya Morocco au USM Alger ya Algeria ambao watacheza majira ya saa nne usiku.