Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua na kupokea taarifa ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI) 2023 kitaifa kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Aprili 30, 2023. Wa pili kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako, kuilia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatuma Mwasa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na Maandalizi kuelekea sherehe za siku ya wafanyakazi duniani zitakazofanyika kesho Mei 1, 2023 kitaifa Mkoani Morogoro katika Uwanja wa Jamhuri.
Ameyasema hayo leo Jumapili (Aprili 30, 2023)alipopokea taarifa na kukagua maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe hizo. Mgeni rasmi atakuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza kamati inayoratibu sherehe hizo na kuwataka kuhakikisha wanakamilisha maeneo ambayo yanahitaji maboresho.
Awali, akitoa taarifa ya maandalizi hayo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi Bi. Fatuma Mwasa amesema maandalizi yamekamilika kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tumaini Nyamhokya amesema kwa upande wa vyama vya wafanyakazi maandalizi yamekamilika na wanamatarajio kuwa mahudhurio yatakuwa makubwa na sherehe hizo kuwa za mafanikio.