Featured Kitaifa

MAAMUZI MAGUMU YA RAIS SAMIA YALIVYOOKOA WATANZANIA 200 SUDAN

Written by mzalendoeditor

 

 
* Aagiza operesheni maalumu iliyofanikisha kuwarejesha Watanzania nyumbani
 
* Tanzania pia ilisaidia kuokoa raia wa mataifa mengine, ikiwemo Marekani, Uingereza, Kenya, Uganda, Sierra Leone, Malawi, Zambia na Msumbiji
 
 
 
UJASIRI, maamuzi magumu na ya haraka ya Rais Samia Suluhu Hassan yamefanikisha kuokolewa kwa maisha ya Watanzania 200 na raia wa nchi nyingine kadhaa kutoka kwenye vita nchini Sudan.

 
Zaidi ya watu 400 wamekufa na maelfu wamekimbia maafa kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea Sudan, ambayo ililipuka kuanzia Aprili 15, 2023.
 
Kufuatia vita hiyo, Rais Samia alifanya maamuzi ya haraka kuagiza ifanyike operesheni maalumu kuwaokoa Watanzania waliokwama Sudan.
 
Maamuzi hayo ya Rais Samia yamesaidia Watanzania 200 kuwasili salama Jijini Dar es Salaam leo asubuhi kwa ndege maalumu ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) namba TC3301.
 
Ndege hiyo ya Boeing Dreamliner iliwabeba Watanzania hao kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa, Ethiopia, hadi Dar es Salaam.
 
Miongoni mwa abiria waliobebwa kwenye ndege hiyo ni wanafunzi 150, watumishi 28 wa ubalozi wa Tanzania Jijini Khartoum na Watanzania wanaoishi Sudan kama Diaspora.
 
Zoezi la uokoaji lilianza kwa Ubalozi wa Tanzania nchini Sudan kukodisha msafara wa mabasi mbao ulisafiri umbali wa kilomita 900 kutoka Khartoum hadi mji wa Gondar, Kaskazini mwa nchi ya Ethiopia.
 
Mabasi hayo yalibeba Watanzania na raia wa nchi kadhaa za kigeni ambao waliomba msaada kwa Tanzania.
 
Miongoni mwa raia wa kigeni walio okolewa na Tanzania wamo raia wa nchi za Marekani, Uingereza, Kenya, Uganda, Sierra Leone, Malawi, Zambia na Msumbiji.
 
Wote kwa pamoja walisafirishwa na Serikali ya Tanzania kwa mabasi kwa siku mbili kutoka Khartoum, Al Qadarif, Metema hadi Gondar (Ethiopia), umbali wa zaidi ya kilometa 900.
 
Baada ya kufika Gondar, raia wa Tanzania walisafirishwa kwa ndege ndogo hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole, Addis Ababa, ambako walichukuliwa na ndege maalumu ya ATCL hadi Dar es Salaam.
 
Uwanja wa ndege wa Gondar ni mdogo, hivyo ilibidi serikali ya Tanzania itafute ndege ndogo mbili ziwachukue abiria hao hadi Addis ili waweze kupanda ndege kubwa ya Dreamliner ya ATCL.
 
Zoezi la uokoaji wa maisha ya Watanzania 200 halikuwa jepesi, kwani viwanja vya ndege nchini Sudan, hususan Khartoum, ambako ndiko kwenye mapigano makali vimefungwa. 
 
Kufuatia siku tatu zilizotolewa za kusitisha mapigano, Aprili 21 hadi 23, serikali ya Tanzania ilitumia mwanya huo kuwasafirisha Watanzania 200 (wanafunzi, watumishi wa Ubalozi, na raia wengine) kupitia Ethiopia kwa magari.
 
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania umemshukuru Rais Samia “kwa kuongoza zoezi hili kwa ujasiri na bila kuchoka, hadi tumeweza kufikia hatua hii.”
 
Pia wizara hiyo imetoa shukurani kwa wote walioshiriki kwenye zoezi la uokoaji, ikiwemo maafisa kutoka Ofisi ya Rais, balozi zote husika za Tanzania, serikali ya Ethiopia na Shirika letu la ndege la ATCL kwa kujituma na kufanya kazi masaa 24.
 
“Tukio hili limetuonyesha umuhimu wa taifa kujitegemea, ikiwa ni pamoja na kuwa na ndege zake.  Hivyo tuunge mkono juhudi za Serikali za kuimarisha amani na usalama na kuleta maendeleo,” ilisema wizara hiyo.

About the author

mzalendoeditor