Featured Kitaifa

SUA KUBORESHA MITAALA KUENDANA NA SOKO LA AJIRA.

Written by mzalendoeditor

Na Farida Mangube Morogoro
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amewataka washiriki wa Mafunzo ya Kujenga Uwezo wa Kuandaa na Kuboresha Mitaala ya Chuo hicho kuyatumia mafunzo hayo kupata Uelewa na kwenda kuandaa Mitaala itakayokidhi na Kuzingatia Mahitaji ya Soko la Ajira.
Amebainisha hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa siku ya pili ambayo ni sehemu ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) yaliyofanyika katika ukumbi wa Mtambuka Kampasi ya Edward Moringe Aprili 25, 2023.
Prof. Chibunda amesema Chuo cha SUA pamoja na mambo mengine ambayo kinayafanya bado kitajikita katika kuboresha Mitaala yake ili kuendeleza kutoa Mafunzo yanayolenga kumjengea mwanafunzi ujuzi, weledi na stadi za kujiajiri na kuajirika (employability skills).
Amesema ili kufikia lengo hilo SUA inahitaji Mitaala inayojumuisha Maarifa ya Kisasa yanayolingana na mahitaji ya soko la ajira inayotilia mkazo umahiri, kukuza stadi za kazi na inayozingatia viwango vya kimataifa hivyo basi amewataka washiriki kuzingatia kwa umakini na kuhakikisha wanapata uelewa wa kina utakaowawezesha kuboresha mitaala ya Chuo.
Kwa upande wake mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo Dkt. Evaristo Mtitu Afisa Mwandamizi wa Elimu ya Juu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mratibu Msaidizi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi (HEET) amesema kati ya mambo manne ambayo Mradi wa HEET unataka kutekeleza moja wapo ni Uuishaji na Uandaaji wa Mitaala.
Amesema wanataka kuanzisha Mitaala isiyopungua 300 na kuboresha iliyopo ili ikidhi mahitaji ya sasa na ya baadae ya Taifa la Tanzania lakini itakayowawezesha wanafunzi kupata Maarifa na Stadi za kuajirika hivyo mafunzo haya kimsingi yataenda kuwajengea uwezo wanataaluma wa SUA katika kuhakikisha kuwa Mitaala wanayoenda kuiboresha inakuwa na sifa ya kumuwezesha mwanafunzi kupata ujuzi stahiki.
“Mwanzoni Mitaala ilielekeza zaidi kwenye kukuza fikra za wanafunzi lakini sio kuwawezesha kupata stadi za kuwafanya kuwa wabunifu, watafutaji au watengeneza ajira na badala yake Mitaala iliwaandaa kutegemea ajira za serikali hivyo naamini kupitia mafunzo haya wanataaluma wa SUA wataenda kwenye idara zao na kuanza kuandaa Mitaala itakayokidhi vigezo”, amesema Dkt. MtituĀ 

About the author

mzalendoeditor