Featured Kitaifa

TAMISEMI YAWASILISHA BAJETI YA MWAKA 2023-2024

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Angellah  Kairuki akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, jana leo 14 Aprili 2023.

Na.Alex Sonna-DODOMA

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imewasilisha bajeti yake bungeni  huku ikiomba kuidhinishiwa zaidi ya Sh trilioni 9.

Akiwasilisha bungeni leo Aprili 14 2023,Waziri wa Tamisemi,Mhe.Angela Kairuki amesema fedha hizo ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya ofisi ,mishahara,mikoa,miradi ya maendeleo tume ya utumishi wa walimu na Halmashauri.

UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2022-2023

Kwenye afya,Mhe.Kairuki  amesema  katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23 ziliidhinishwa Shilingi Bilioni 143.15 kupitia ruzuku ya Serikali Kuu kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Afya ya Msingi.

Amesema hadi Februari, 2023 Shilingi Bilioni 124.10 zimepokelewa sawa na asilimia 86.69 ya fedha iliyoidhinishwa.

Kairuki amesema Shilingi Bilioni 15.50 ziliidhinishwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali 31 za Halmashauri zilizoanza ujenzi katika Mwaka wa Fedha wa 2020/21 ambapo kila Halmashauri iliidhinishiwa Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje na maabara.

Amesema hadi Februari, 2023 Shilingi Bilioni 13.50 zimekwishatolewa, sawa na asilimia 87.09 na ujenzi upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Amesema Shilingi Bilioni 25.15 ziliidhinishwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali 28 za Halmashauri zilizoanza ujenzi katika Mwaka wa Fedha wa 2021/22.

“Ujenzi huo ulihusisha majengo ya wodi 3 za wanaume, wanawake na watoto pamoja na jengo la kuhifadhia maiti,”amesema Mhe.Kairuki

Amesema hadi Februari, 2023 zimepokelewa Shilingi Bilioni 23.90, sawa na asilimia 95.03 ambapo ujenzi wa majengo upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

 HOSPITALI KONGWE

Aidha,Kairuki amesema shilingi Bilioni 16.55 ziliidhinishwa kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali kongwe 19 za Halmashauri.

Amesema hadi Februari, 2023 zimepokelewa Shilingi Bilioni 16.55, sawa na asilimia 100 ya fedha zilizoidhinishwa ambapo ukarabati wa hospitali tisa  umeanza na kwa upande wa hospitali kumi  ukarabati upo katika hatua za awali.

ZAHANATI ZA NGUVU YA WANANCHI

Kairuki amesema Shilingi Bilioni 15 ziliidhinishwa kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 300 ya zahanati yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.

Amesema hadi Februari, 2023 Shilingi Bilioni 14.60 zimepokelewa, sawa na asilimia 97.33 na ukamilishaji upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Aidha, Shilingi Bilioni 1 ziliidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo 2 vya afya katika Halmashauri za Wilaya za Msalala na Ukerewe ambapo hadi Februari, 2023 Shilingi Bilioni 1 sawa na asilimia 100 zimepokelewa na ujenzi upo katika hatua mbalimbali.

Vilevile, hadi kufikia Februari, 2023 jumla ya wagonjwa wa nje (OPD) 16,143,151 na wagonjwa wa ndani waliolazwa (IPD) 416,628 walipatiwa huduma katika vituo vya kutolea huduma za Afya ya Msingi.

Pia, kati ya akina mama wajawazito 1,227,234 waliojifungua, akina mama 1,146,510 sawa na asilimia 93.4 walijifungua kwa njia ya kawaida na akina mama 80,724 sawa na asilimia 6.6 walijifungua kwa njia ya upasuaji.

VIFAA TIBA

Waziri Kairuki amesema Shilingi Bilioni 69.95 ziliidhinishwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba.

Amesema kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 15.15 ni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa  kwa zahanati 300, Shilingi Bilioni 47.70 kwa Vituo vya Afya 159 na Shilingi Bilioni 7.10 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba vya afya ya kinywa, meno na macho kwa hospitali za Halmashauri 71 zilizokamilika.

Hadi Februari, 2023 jumla ya Shilingi Bilioni 54.55 zimepokelewa, sawa na asilimia 77.98.

Amesema kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 11.95 ni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa zahanati,

Kairuki amesema Shilingi Bilioni 36.75 kwa ajili ya Vituo vya Afya na Shilingi Bilioni 5.85 kwa ajili ya vifaa tiba vya kinywa na macho kwa Hospitali za Halmashauri 71.

USTAWI JAMII

Kairuki amesema ili kuimarisha huduma za Ustawi wa Jamii kwa makundi maalum, hadi Februari, 2023 Ofisi ya Rais – TAMISEMI imefanikiwa kuwatambua jumla ya Watu Wenye Ulemavu 10,035 ambapo Wanawake ni 6,100 na Wanaume 3,935.

Miongoni mwa Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi 2,400 kati yao Wanawake ni 1,300 na Wanaume 1,100; Watu Wenye Ulemavu wa Viungo 5,233 ambapo Wanawake ni 3,133 na Wanaume 2,100;Wasioona 510 ambapo Wanawake ni 203 na Wanaume 307.

Amesema  Viziwi 1,500 kati yake Wanawake ni 785 Wanaume 715; na Watu Wenye Ulemavu wa Akili 392 ambapo Wanawake ni 281 Wanaume.

HUDUMA ZA LISHE

Kairuki amesema Kiwango kikubwa cha udumavu kimebainika katika Mikoa ya Iringa asilimia 56.9; Njombe asilimia 50.4; Tabora asilimia 33.1 na Dar es Salaam asilimia 18.4.

Hivyo, Ofisi ya Rais-TAMISEMI inaendelea kufanya usimamizi shirikishi na uratibu wa afua katika Mikoa hiyo ili kuhakikisha kiwango cha udumavu

“Katika kutekeleza agizo la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kufanya utafiti wa visababishi vya udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano katika Mikoa inayozalisha vyakula kwa wingi hapa nchini.

“Utafiti unafanyika kwa kushirikiana na Taasisi ya Big Win Philantropy kutoka nchini Marekani kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika. Utafiti unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa Mei, 2023 ambao unafanyika katika Mikoa nane.

“ Utafiti huo unafanyika katika Mikoa sita  ya Tanzania Bara ambayo ni Njombe, Iringa, Tabora, Dar es Salaam, Geita na Mtwara pamoja na Mikoa miwili (2) ya Zanzibar ambayo ni Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba,” amesema Waziri Kairuki.

USIMAMIZI NA UENDESHAJI WA ELIMUMSINGI NA SEKONDARI

Waziri Kairuki amesema katika mwaka wa masomo wa 2022 wanafunzi wapya wa Darasa la Awali walioandikishwa ni 1,411,810, sawa na asilimia 103.52 ya lengo la kuandikisha wanafunzi 1,363,834.

Amesema katika Mwaka 2023, jumla ya wanafunzi 1,500,227 wameandikishwa sawa na asilimia 109.37 ya lengo la kuandikisha wanafunzi 1,371,690 wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum 2,411 ambapo wasichana ni 1,211 na wavulana 1,200.

Amesema uandikishwaji huo ni ongezeko la wanafunzi 88,417 sawa na asilimia 3.38 ikilinganishwa na wanafunzi walioandikishwa kwa kipindi kama hiki kwa Mwaka wa 2022.

“Ongezeko hili limetokana na uhamasishaji wa jamii, ujenzi wa vituo shikizi na kuendelea kutoa ElimuMsingi Bila Ada,”amesema Waziri Kairuki.

DARASA LA KWANZA

Amesema katika Mwaka wa masomo wa 2022 wanafunzi 1,592,375 walitarajiwa kuandikishwa Darasa la Kwanza, ambapo walioandikishwa ni wanafunzi 1,726,165, sawa na asilimia 108.40 ya lengo.

Katika Mwaka 2023 wanafunzi wa Darasa la Kwanza walioandikishwa hadi Februari, 2023 ni 1,786,485, ambapo wasichana 917,211 na wavulana ni 869,274.

Amesema uandikishwaji huo ni sawa na asilimia 109.07 ya lengo la kuandikisha wanafunzi 1,637,897 na ni ongezeko la wanafunzi 60,320, sawa na asilimia 3.49, ikilinganishwa na wanafunzi walioandikishwa kwa kipindi kama hicho kwa Mwaka wa 2022.

Kairuki amesema Ongezeko hilo limetokana na uhamasishaji wa jamii, ujenzi wa vituo shikizi na kuendelea kutoa ElimuMsingi Bila Ada.

ELIMU MAALUM

Amesema Kati ya wanafunzi walioandikishwa wenye mahitaji maalum ni 4,741 ambapo wasichana ni 2,097 na wavulana ni 2,644.

“Lengo ni kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapatiwa huduma bora ya elimu kulingana na Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2022– 2026,”amesema Kairuki.

KIDATO CHA KWANZA

Waziri Kairuki amesema jumla ya wanafunzi 1,076,037 ambapo wasichana 560,118 na wavulana ni 515,919 walichaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka wa 2023.

Amesema hadi Februari, 2023 wanafunzi 1,003,982 ambapo wasichana 520,332 na wavulana ni 483,650 wameandikishwa sawa na asilimia 93.3 ya wanafunzi waliochaguliwa.

“Kati ya wanafunzi walioandikishwa, wanafunzi wenye mahitaji maalum ni 2,411 ambapo wasichana 1,211 na wavulana ni 1,200,”amesema Kairuki.

SEKONDARI

Waziri Kairuki amesema Ofisi yake  imeendelea kusimamia uchaguzi wa wanafunzi waliofaulu mtihani wa kidato cha nne ambapo jumla ya wanafunzi 90,898 kati yao wasichana 43,155 na wavulana 47,743, sawa na asilimia 52.41 ya wanafunzi 173,422 wenye sifa walichaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika shule 508 za Serikali.

Amesema kati yao, wanafunzi wenye mahitaji maalumu walikuwa ni 481 wakiwemo wasichana 204 na wavulana 277.

Amesema Kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano, wanafunzi 36,390 wakiwemo wasichana 15,327 na wavulana 21,063 sawa na asilimia 40.03 walichaguliwa kusoma tahasusi za Sayansi na Hisabati.

Amesema  wanafunzi 54,508 wakiwemo wasichana 27,828 na wavulana 26,680 sawa na asilimia 59.97 walichaguliwa kusoma tahasusi za masomo ya Sanaa na Biashara.

MAHITAJI YA WALIMU

 

Kairuki amesema hadi Februari, 2023 kuna jumla ya Shule za Msingi 17,181 zenye jumla ya wanafunzi 12,362,571 ambapo wasichana ni 6,269,643 na wavulana ni 6,092,928 kati yao wenye mahitaji maalum ni 65,641 ambapo wasichana ni 28,116 na wavulana ni 37,525.

Aidha, zipo Shule za Sekondari 5,540 zikijumuisha 4,211 za Serikali na Shule 1,329 za binafsi zenye jumla ya wanafunzi 2,823,588 ambapo wasichana ni 1,476,369 na wavulana ni 1,347,219 wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum 13,142 ambapo wasichana ni 6,720 na wavulana ni 6,422.

Waziri Kairuki amesema hadi Februari, 2023 mahitaji ya walimu katika Shule za Msingi ni 362,189 kwa kutumia uwiano wa 1:45 (Mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45) ambapo walimu waliopo ni 175,864 na upungufu ni 186,325 sawa na asimilia 51.44 ya mahitaji.

Aidha, mahitaji ya walimu kwa Shule za Sekondari ni 174,632 ambapo waliopo ni 84,700 na upungufu ni walimu 89,932 sawa na asilimia 51.5.

Amesema mahitaji ya walimu  kwa shule za Sekondari yanatokana na masomo yanayofundishwa.

Vilevile, mahitaji ya walimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa Shule za Msingi ni walimu 4,462 ambapo waliopo ni 1,517 na upungufu ni walimu 2,945 sawa na asilimia 66.

Amesema Serikali inaendelea kuajiri walimu kulingana na hali ya uchumi inavyoruhusu.

MAPATO YA NDANI

Amesema katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23 Halmashauri ziliidhinishiwa kukusanya Shilingi Trilioni 1.01 kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato ya ndani ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 148.42, sawa na asilimia 17.18 ikilinganishwa na bajeti ya Shilingi Bilioni 863.85 ya Mwaka wa Fedha wa 2021/22.

Hadi Februari, 2023 Halmashauri zimekusanya jumla ya Shilingi Bilioni 625.31 sawa na asilimia 62 ya makisio kwa Mwaka wa Fedha wa 2022/23.

Amesema makusanyo haya ni ongezeko la Shilingi Bilioni 9.70 sawa na asilimia 1.57 ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi Bilioni 615.61 yaliyokusanywa kwa kipindi kama hiki katika Mwaka wa Fedha wa 2021/22.

MIKAKATI YA KUKUSANYA MAPATO

Kairuki amesema Tamisemi itaendelea kuzisimamia Halmashauri ili ziongeze wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Ameitaja iliyowekwa ni pamoja na kuwajengea uwezo maafisa wanaokusanya mapato, kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato na utambuzi wa fursa na uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato.

 Aidha, Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaendelea kupima utendaji wa Halmashauri kwa kutumia vigezo vya upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo kwa kuzingatia asilimia 70,60,40,20 na vigezo vingine vilivyowekwa.

KERO ZA WANANCHI

Aidha,Waziri Kairuki amesema katika kuendelea kuimarisha Utawala Bora, Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI zimeendelea kutekeleza dhana ya ‘‘TAMISEMI ya Wananchi’’.

Amesema Katika kutekeleza dhana hiyo, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeendelea kuimarisha Kituo cha Huduma ya Mawasiliano kwa Mteja (Call Centre) kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi bila ya kuhitaji kusafiri kuja Ofisi ya Rais – TAMISEMI Dodoma.

USIMAMIZI WA FEDHA

Kairuki amesema Tamisemi  imeendelea kutoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu usimamizi wa fedha kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali ya usimamizi wa fedha inayotolewa mara kwa mara ili kuwezesha ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za umma.

Amesema lengo ni kuhakikisha kuwa mapato yanakusanywa kwa ufanisi na kuziba mianya ya kuvuja kwa makusanyo na kudhibiti matumizi.

“Katika kuhakikisha kunakuwa na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imefanyia kazi changamoto zilizokuwepo katika mfumo wa mapato wa Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS) kwa kusanifu na kujenga mfumo mpya wa TAUSI ambao umeanza kutumika katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23,”amesema.

Amesema hadi Februari, 2023 Halmashauri 169 zimeanza kutumia mfumo wa TAUSI ambao umeboreshwa kulinganisha na mfumo wa awali wa Local Government Revenue Collection Information System uliotumika kwa zaidi ya miaka 7.

“Mfumo huu utadhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kudhibiti matumizi hususan matumizi ya fedha mbichi,”amesema Kairuki

BARABARA

Amesema kazi za matengenezo ya barabara za Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) huongozwa na mwongozo wa matumizi ya fedha zitokanazo na tozo ya mafuta chini ya Bodi ya Mfuko wa Barabara.

Amesema  Mwongozo huo unaelekeza kuwa matengenezo ya miundombinu ya barabara zenye hali nzuri na wastani zinafanyiwa matengenezo kwa asilimia 100 kwa lengo la kuhakikisha kuwa uwekezaji uliofanyika unatunzwa ili ufikishe umri wake uliokusudiwa.

MPANGO WA BAJETI NA VIPAUMBELE

Ofisi ya Rais- TAMISEMI imepanga kutekeleza Mpango na Bajeti kwa kuzingatia vipaumbele vya kusimamia masuala ya utawala bora, kukuza demokrasia, ushirikishwaji wa wananchi na Ugatuaji wa Madaraka kwa Umma (D by D).

Pia,kuratibu maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwenye Vijiji 12,318, Mitaa 4,263 na Vitongoji 64,361 katika Halmashauri 184 utakaofanyika mwaka 2024.

“Kuratibu suala la ulinzi na usalama katika Mikoa na Wilaya,Kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya jamii katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za utoaji wa Huduma za Afya ya Msingi, Ustawi wa Jamii na Lishe katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa,”amesema

Pia,Kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za utoaji wa ElimuMsingi na Sekondari katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa ikijumuisha utekelezaji wa ElimuMsingi na Sekondari Bila Ada.

Vilevile,Kuratibu na kusimamia Mkakati wa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi katika Mamlaka za

Serikali za Mitaa,Kuratibu ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya Barabara, Usafirishaji, Afya ya Msingi, ElimuMsingi na Sekondari na majengo ya utawala katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa;

Pia,Kuratibu na kusimamia shughuli za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

About the author

mzalendoeditor