Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara akifungua mafunzo hayo.
Mwakilishi wa Barrick North Mara,Zachayo Makobero,akiongea wakati wa ufunguzi
Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada
Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada
Baadhi ya washiriki katika picha ya pamoja na viongozi na wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Baadhi ya washiriki katika picha ya pamoja na viongozi na wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
***
-Mafunzo yaendeshwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
VIONGOZI wa vijiji 11 na kata tano zinazozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, wameanza mafunzo ya kuibua na kusimamia utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameanza mjini Tarime leo Aprili 12, 2023,yanaendeshwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Saaam, chini ya udhamini wa mgodi wa Barrick North Mara.
Mbali na wenyeviti, madiwani na maafisa watendaji wa vijiji na kata, mafunzo hayo yanawashirikisha pia wataalamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara wapatao 63 kwa ujumla wao.
Afisa Mwandamizi wa Mahusiano ya jamii wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Zachayo Makobero. amesema lengo ni kuwajengea viongozi hao uwezo wa kuibua na kusimamia miradi inayotekelezwa kutokana na fedha zinazotolewa na Barrick kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Huduma za Kijamii (CSR).
“Lengo la mgodi wa North Mara ni kuwajegea uwezo wa kuibua na kusimamia miradi ya CSR, ikiwemo ya kimkakati ili itekelezwe kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati, lakini pia iwe na tija na manufaa makubwa kwa jamii,” amesema Makobero.
Akifungua mafunzo hayo, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara amesema yatasaidia kuepusha ukwamaji na ubabaishaji wa wa miradi ya kijamii inayotekelezwa kutokana na fedha za CSR.
“Hii ni nafasi muhimu sana ya kujifunza ili tuweze kusonga mbele. Watu wa Tarime ili watuelewe wanataka kuona miradi inatekelezwa vizuri, wanataka kuona fedha za CSR zinatumika vizuri,” amesema Mbunge Waitra ambaye ndiye amekuwa mgeni rasmi wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Washiriki wameishukuru Barrick North Mara wakisema mafunzo hayo yatakuwa chachu ya ufanisi katika uibuaji na usimamizi wa utekelezaji wa miradi inayotokana na fedha za CSR.
“Hili ni jambo zuri sana, mafunzo haya yana maana kubwa kwetu kwa sababu tumekuwa tukipata tuhuma mbalimbali kutokana na kukosa mafunzo ya usimamizi wa miradi,” amesema Simion Kiles Samwel, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
“Ninaushukuru sana mgodi wa Barrick North Mara, kwa sababu tangu CSR ianze hatujawahi kupata mafunzo kama haya, tunaamini yatatusaidia sana kuibua miradi mingi ikiwemo ya kiuchumi na kuisimamia vizuri,” amesema Sylvanus Gwiboha, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
“Tunuishuku Barrick North Mara, kwa kufadhili mafunzo haya, tukirudi maeneo yetu ya uongozi tutafundisha wengine ambao hawakupata nafasi ya kuyahudhuria,” amesema Maria Wankyo Sylvester, Diwani wa Viti Maalum kutoka kata ya Mwema.
“Mafunzo haya yatatuwezesha kujua muongozo wa kuibua miradi yenye tija na kusimamia utekelezaji wake kwa weledi,” amesema Chacha Makuri, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyakunguru.
“Tunakwenda kujua namna bora ya kusimamia miradi ya CSR. Mimi kwa kweli ninawashukuru Barrick North Mara kwa kuona umuhimu wa kutuletea haya mafunzo ili tupate uelewa wa pamoja,” amesema James Magige Wambura, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyamwaga.
Wakufunzi/ wawezeshaji wa mfunzo hayo ni wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM); ambao ni Dkt. Hezron Makundo wa Idara ya Taaluma za Maendeleo, Dkt. Theresia Busagara wa Idara ya Fedha na Dkt. Fred Okongi wa Idara ya Masoko.