WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kusaini mkataba wa kuanzisha Kituo cha Huduma za Binadamu na Operesheni za Dharura cha Kanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
“Lengo la kuanzisha kituo hicho ni kusimamia utoaji wa huduma na misaada ya kibinadamu kwa nchi wanachama. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, masuala ya majanga hayana mipaka na hayana muda na yanahitaji jitihada za pamoja katika kuyashughulikia,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 5, 2023) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.
“Kama mtakumbuka, katika kuendeleza uhusiano na nchi nyingine, hivi karibuni nchi yetu imeungana na mataifa mengine duniani kutoa misaada ya kibinadamu kwa nchi zilizopatwa na maafa makubwa yaliyosababisha vifo na majeruhi, uharibifu wa mali na mazingira. Nchi hizo ni Malawi iliyokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Freddy kilichotokea tarehe 13 Machi, 2023 na Uturuki iliyokumbwa na tetemeko la ardhi Februari, mwaka huu,” amesema.
Ameitaja misaada iliyotolewa Malawi kuwa ni tani 1,000 za mahindi, mablanketi 6,000, mahema 50, fedha taslimu sh. milioni 705, dawa za binadamu na helikopta mbili kwa ajili ya kusaidia uokoaji. Vilevile, Uturuki ilipewa dola za Marekani milioni moja.
Akielezea utekelezaji wa shughuli za maafa kwa mwaka 2022/2023, Waziri Mkuu Majaliwa amesema wajumbe 555 wa Kamati za Usimamizi wa Maafa na Waratibu wa Maafa walipatiwa mafunzo ya kuimarisha uwezo wa utendaji kazi katika mikoa ya Arusha, Morogoro, Kilimanjaro, Lindi, Mtwara na Singida.
“Pia wavuvi 344 katika mwambao wa Ziwa Victoria na vijana 40 wa kujitolea katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Songwe na Tabora walipata mafunzo ya uokoaji, yaliyowaongezea uwezo wa kukabiliana na maafa kwa wakati,” amesema.
Amesema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itaendelea na ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa jijini Dodoma na kuimarisha maghala ya vifaa vya misaada ya kibinadamu kwa kuongeza vifaa na kuendelea kutoa misaada kwa waathirika wa maafa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ameitaka kila wizara na taasisi wajiandae kwa vifaa vya kukabiliana na maafa kulingana na mahitaji ya wizara au taasisi husika.
Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe sh. 173,733,110,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 121,364,753,320/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 52,368,356,680/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.
Pia ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh. 165,627,897,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 160,458,877,000/- ni za matumizi ya kawaida na sh. 5,169,020,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.