WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda madawati 1,393 ya ulinzi na usalama wa mtoto katika shule za msingi na sekondari ili kupinga ukatili dhidi ya watoto shuleni na nje ya shule.
Mheshimiwa Majaliwa amesema madawati hayo yameundwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwenye mikoa ya Rukwa, Arusha, Tanga, Dar es Saalam, Pwani, Shinyanga, Dodoma na Geita.
Vilevile, Waziri Mkuu amesema mabaraza 560 ya watoto yameundwa kwa lengo la kutoa fursa kwa watoto kutoa maoni yao kwa uhuru na kuwajengea uwezo wa kujiamini, kujieleza na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu haki na ustawi wao.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 5, 2023) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024 bungeni jijini Dodoma.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi wote wa Serikali, dini, kimila na vyama vya siasa kukemea kwa nguvu zote ushiriki wa jamii katika matendo yasioendana na mila, tamaduni na desturi za Watanzania.
“Hii ni pamoja na wazazi na walezi wote kushirikiana na Serikali katika makuzi na malezi bora ya watoto yatakayowaepusha na vitendo viovu. Serikali imeendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika ulinzi na usalama wa mtoto ili kutokomeza ukatili dhidi yao.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi watalii milioni 2.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 199.5.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeendelea kuwa hifadhi bora duniani ambapo kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2022 imepata tuzo ya dhahabu ya utoaji wa huduma bora iliyotolewa na European Society for Quality Research.
Amesema Serikali imeendelea kuimarisha sekta za maliasili na utalii kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali ili kukuza utalii, kuitangaza nchi yetu na vivutio vyake kitaifa na kimataifa pamoja na kuimarisha mchango wa sekta hizo kwenye pato la Taifa.
Amesema katika mwaka 2022/2023, programu mbalimbali zimeendelea kutekelezwa ikiwemo Programu ya Tanzania – The Royal Tour na utangazaji wa vivutio vya utalii kupitia matukio mbalimbali na vyombo vya habari ikiwemo Tanzania Safari Channel.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kutokana na jitihada hizo, idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kutoka watalii 922,692 katika mwaka 2021 hadi kufikia watalii takriban milioni 1.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 57.7.
Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2023/2024 Serikali itaendelea kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo utalii wa fukwe, mikutano na matukio, meli, michezo na utamaduni.
Vievile, itaendelea kuimarisha miundombinu katika maeneo ya hifadhi, kukarabati majenzi ya kale na kuyatangaza kidijitali pamoja na kutekeleza mikakati ya kuongeza thamani ya mazao ya misitu.