Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya 2023/2024, bungeni jijini Dodoma, Aprili 5, 2023. Wengine kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Wziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
* Ni ya ujenzi na ukarabati wa mabwa na skimu za umwagiliaji
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka 2022/2023, Serikali imesaini mikataba 31 yenye thamani ya shilingi bilioni 284.14 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji.
“Mikataba hiyo inahusu ujenzi wa mabwawa nane, skimu mpya 13 na ukarabati wa skimu 17, hivyo kutaongeza eneo la umwagiliaji na kufikia hekta 778,210.6 kutoka hekta 727,280 mwaka 2021/2022.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema pamoja na changamoto za hali ya hewa, hali ya upatikanaji wa chakula cha kutosha katika maeneo yote nchini imeendelea kuimarika.
Amesema katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023, uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa ulikuwa tani milioni 17.4 ikilinganishwa na mahitaji halisi ya tani milioni 15.1.
Uzalishaji huo umeihakikishia nchi utoshelevu wa chakula kwa asilimia 115 kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024. Hata hivyo amesisitiza juu ya matumizi bora ya chakula.
“Nitoe wito kwa Watanzania kuhifadhi mazao ya nafaka kwani utengamano wa hali ya chakula nchini umeendelea kuwepo kutokana na ziada inayotokana na mazao yasiyo ya nafaka.”
Akizungumzia kuhusu maeneo yaliyokuwa na changamoto ya chakula Waziri Mkuu amesema hadi Januari, 2023, tani 29,084.21 za mahindi zilisambazwa katika Halmashauri 59 zilizokuwa na upungufu wa chakula kwa mwaka 2022/2023.
“Mahindi hayo yaliuzwa kwa bei ya chini ya soko ili kuimarisha upatikanaji wa chakula katika maeneo hayo. Pia Serikali imeendelea kuratibu upatikanaji wa mbolea, mbegu bora na viuatilifu kwa wakati ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo.”
Amesema hadi Februari, 2023, upatikanaji wa mbolea umefikia tani 407,333 sawa na asilimia 58.33 ya mahitaji ya tani 698,260. Upatikanaji huo umechangiwa na tani 28,672 zilizozalishwa ndani, tani 251,697 zilizoingizwa , zikiwemo kutoka nje ya nchi na tani 126,963 ambazo ni bakaa ya msimu wa 2022/2023.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuhakikisha mbolea iliyobaki inapatikana na kusambazwa kwa wakulima kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya kila mkoa na kupunguza makali ya bei.
Akizungumzia kuhusu changamoto ya uzalishaji wa mafuta ya kula, Waziri Mkuu amesema Serikali imetoa tani 591.1 za mbegu za alizeti kwa wakulima wa Mikoa ya Singida, Dodoma, Kagera, Mbeya na Mwanza kwa utaratibu wa ruzuku.
Amesema hatua hiyo, itasaidia kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini na kupunguza matumizi ya fedha nyingi za kigeni zinazotumika kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imegawa lita 63,606 za viuatilifu katika mikoa 15 nchini ili kuthibiti viwavijeshi, nzi wa matunda na ndege waharibifu aina ya Quelea quelea. “Hatua hiyo imesaidia kuokoa ekari 159,015 za mazao mbalimbali yakiwemo mahindi na mpunga.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kuhakikisha kasi[Ma1] ya kutoa huduma kwa wakulima inaongezeka, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za ugani kwa kutoa mafunzo na vitendea kazi kwa maafisa ugani na kuanzisha Kituo cha Huduma kwa Wateja.
Amesema kituo hicho kimeshatoa huduma ya ushauri na taarifa za kilimo kwa wakulima na wadau wapatao 12,248. “Aidha, kwa kupitia mfumo wa M-Kilimo, wakulima 7,269,101 na Maafisa Ugani 9,985 wamesajiliwa kwa ajili ya huduma za ushauri wa kitaalamu. Teknolojia hii itawawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kuyafikia masoko ya mazao kwa njia ya simu.”