Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatma Toufiq akiwasilisha taarifa ya kamati kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa mwaka 2022/23 pamoja na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2023/24.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akiteta jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Bunge Mhe. Jenista Mhagama wakati wa Mkutano wa 11 wa Bunge la 12 kikao cha pili, leo Aprili 5, 2023 Bungeni, jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu, DODOMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeshauri serikali iongeze bajeti ya programu ya kukuza ujuzi nchini ili kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.Fatuma Toufiq ametoa ushauri huo Aprili 5, 2023 alipokuwa akiwasilisha taarifa bungeni kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa mwaka 2022/23 pamoja na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2023/24.
Amesema katika mpango huo vijana 681,000 wanaotakiwa kupata mafunzo ya ujuzi katika kipindi cha miaka mitano.
Aidha, amesema kamati imeshauri serikali ihakikishe Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unatangazwa ili kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kuwezeshwa kupitia mfuko huo.
“Kamati inaipongeza serikali kwa kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kilimo unaowasaidia kujiajiri, kujiingizia kipato na kuongeza uzalishaji wa chakula,”amesema.
Pia, Kamati imeshauri kuwa Serikali iendelee kuweka mkakati maalumu wa kuwajumuisha watu wenye ulemavu kwenye Programu ya Taifa ya kukuza ujuzi nchini na programu zingine ili kuhakikisha kuwa fursa kwa watu wenye ulemavu zinaimarishwa.
Kadhalika, Mhe. Toufiq ameshauri fedha zinazotengwa kwa ajili ya mafunzo ya watumishi zitumike kuwapatia watumishi mafunzo ya ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.