Featured Kitaifa

RASIMU YA MABADILIKO YA MITALAA NA MAPITIO YA SERA YAKAMILIKA WADAU KUTOA MAONI YA MWISHO

Written by mzalendoeditor

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema tayari rasimu za mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo na ile ya mitalaa zimekamilika na wakati wowote itatolewa kwa wadau ili waone kilichopendekezwa na kutoa maoni yao mengine ya mwisho.

Hayo yamesemwa hivi karibuni Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda wakati akizungumza katika kikao cha kuwapitisha wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo katika rasimu hizo.

Mhe. Prof. Adolf Mkenda aliongeza kuwa lengo la kufanya mapitio na mabadiliko hayo ni kutekeleza ahadi aliyotoa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na mabadiliko ya mitaala ili kuwezesha kutoa elimu ujuzi na pia kuwezesha sera na mitaala kuakisi mahitaji ya sasa na baadae .

Waziri huyo ameongeza kuwa katika kutekeleza hilo Serikali iliunda kamati mbili, Kamati ya mapito ya Sera na ya Mabadiliko ya Mitaala ambazo zilifanya kazi ya kukusanya maoni ambayo yalichambuliwa na wataalam na kupata rasimu.

“Kazi ya kwanza ya Kamati hizi ilikuwa kukusanya maoni ya wananchi na baadaye maoni hayo yalifanyiwa uchambuzi na kuwezesha kupatikana kwa rasimu ya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo toleo la Mwaka 2023 na Rasimu ya Mitaala mipya,” amesema Prof. Mkenda.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa Wizara itafanya kongamano la siku tatu ambapo itatoa rasimu hizo kwa wadau ili wapitie mapendezo na pia watapata nafasi ya kutoa maoni kabla ya kufikia hatua ya mwisho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Prof. Kitila Mkumbo ameishukuru Wizara kwa kuona umuhimu wa kuipitisha Kamati hiyo katika rasimu hizo ili nao waweze kutoa maoni yao.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa kazi iliyofanyika ni kubwa sana na ambayo inapaswa kupongezwa kwani kupatikana kwa toleo jipya la Sera ya Elimu itawezesha wabunge kufanya kazi wakiwa na nyenzo.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko amesema maboresho yatakayofanyika yanakwenda kuinua ubora wa elimu na kuitaka wizara baada ya kuridhiwa basi utekelezaji wake uanze mara moja huku akiitaka kuanza kutenga fedha katika bajeti za kuanza maandalizi ya utekelezaji huo.
.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amewaambia wajumbe wa Kamati hiyo kuwa maboresho hayo hayataishia katika ngazi ya elimu msingi pekee bali yatakwenda mpaka ngazi ya elimu ya juu.

About the author

mzalendoeditor