Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Prof.Joyce Ndalichako,akizungumza leo   Machi 30, 2023 kuelekea uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2023 mkoani Mtwara.

Na Mwandishi Wetu, Mtwara
WAZIRI Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua mbio za Mwenge wa Uhuru Aprili mosi, 2023 katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara ambazo kwa mwaka huu zinalenga kuhimiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Prof.Joyce Ndalichako ameyasema hayo Machi 30, 2023 alipokuwa akitoa maelezo ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2023 mkoani Mtwara.

Amesema Mwenge huo utakimbizwa kwenye Mikoa 31 katika Halmashauri 195 ukiwa na ujumbe ‘Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa’.

“Ujumbe Mkuu wa Mwenge unalenga pia kuwaelimisha na kuwakumbusha wananchi juu ya mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira na athari zake katika vyanzo vya maji, ikolojia na uhai wa viumbe, lengo kuu ni kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika harakati za kuhifadhi Mazingira na kutunza vyanzo vya Maji,”amesema.

Pamoja na hayo, Mhe.Ndalichako amesema mbio hizo zitaendelea kuelimisha na kuihamasisha jamii kushiriki mapambano dhidi ya rushwa, VVU/UKIMWI, madhara ya matumizi ya dawa za kulevya , ugonjwa wa malaria na umuhimu na uzingatiaji wa lishe bora kwa afya imara.

Pia amesema mbio hizo zitaendelea kuhamasisha wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao na wadau wa maendeleo katika kubuni na kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo na kuhamaisha na kuimarisha Muungano wa Tanzania.

Previous articleNAIBU WAZIRI KIPANGA ATAKA MKANDARASI KUONGEZA KASI UJENZI JENGO LA TAEC DAR ES SALAAM
Next articleMAAFISA MAWASILIANO NA UHUSIANO SERIKALINI WAASWA KUTANGAZA MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MKUMBI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here