Featured Kitaifa

WAZIRI DKT. GWAJIMA AWAPA MBINU UWT MIKOA, KUKABILI MASUALA YA UKATILI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akiwasilisha mada kuhusu mapambano ya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto nchini katika Mafunzo ya viongozi wa Umoja wa Wanawake Chama cha Mapinduzi (UWT) ngazi ya Mikoa na Wilaya inayofanyika jijini Dodoma tarehe 21-22 Machi, 2023.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akifuatilia mada na mijadala wakati wa mafunzo kwa viongozi wa Umoja wa Wanawake Chama cha Mapinduzi (UWT) ngazi ya Mikoa na Wilaya inayofanyika jijini Dodoma tarehe 21-22 Machi, 2023.

Baadhi ya Viongozi wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) ngazi za Mikoa na Wilaya wakifuatilia mada mbalimbali kwenye Mafunzo yanayofanyika jijini Dodoma tarehe 21-22 Machi, 2023.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM)

Na WMJJWM, Dodoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa viongozi hususani wanawake kubeba ajenda ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia na watoto kwenye vikao vyote kuanzia kwenye maeneo yao.

Waziri Dkt. Gwajima ametoa wito huo alipokuwa akiwasilisha mada ya mapambano ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwenye mafunzo ya Wajumbe wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Viongozi wa UWT ngazi ya Mikoa na Wilaya jijini Dodoma Machi 21-22, 2023.

Amesema Wanawake Viongozi wana nafasi ya kuzungumzia ajenda ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto kwani, pamoja na takwimu kuonesha wanawake wanafanyiwa ukatili, kuna baadhi ya wanawake wanakatili watoto au wanakatili wengine au wanajikatili wenyewe.

“Mila na Desturi nyingine zinatufanya tufanyiane ukatili wenyewe wanawake mfano
ukeketaji, kung’oa meno watoto, kuwafanyia urembo usio na tija watoto na kuwaumiza huku wengine kutovaa mavazi ya staha hivyo, umefika wakati wa kuongea haya kama tunahitaji kuleta mabadiliko ya ulimwengu huu” amesisitiza Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima amefafanua kuwa wapo baadhi ya wazazi au walezi wanawasuka watoto nywele tena kwa maumivu makali urembo ambao hauna tija kwa watoto zaidi unawasababishia athari kwenye ubongo jambo ambalo ni ukatili wa Wanawake kwa watoto wa kike.

Aidha, Dkt. Gwajima amewahimiza viongozi hao kuhakikisha wanaweka mikakati kwenye jamii namna ya kupambana kutokomeza ukatili na malezi duni yanayochangia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili huku akibainisha kuwa yanaleta athari za kimwili, kisaikolojia na kiuchumi.

Ameongeza pia kuwa, utandawazi umekuwa changamoto inayoathiri mifumo ya malezi kuanzia nyumbani, shuleni na maeneo mengine hali iliyoathiri uimara wa mifumo ya wakala wa malezi ikiwemo familia, shule, Dini na jamii kwa ujumla.

Akielezea hali halisi ya ukatili nchini, Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kwamba mwaka 2022 matukio 12,163 ya ukatili kwa watoto yameripotiwa ukilinganisha na 11,499 mwaka 2021 ambapo ubakaji ni 6,335, ulawiti 1555, mimba za utotoni 1557, kuzorotesha masomo 808 na mashambulizi 231.

Hata hivyo Waziri Dkt. Gwajima ameipongeza mikoa ya Arusha, Mbeya, Kinondoni, Tanga na Mwanza kwa kuwa na mifumo imara inayotoa elimu kwa jamii na kufuatilia vitendo vya ukatili kwani katika kuelimisha jamii namna ya kuzuia na kutoa taarifa Ili hatua za kisheria zichukuliwe, ndiyo itawezekana kutokomeza.

Amesisitiza kuwa, matukio mengi ya ukatili hufichwa na jamii maeneo ambako hakuna elimu na mifumo thabiti hivyo, manusura hukosa huduma na haki.

About the author

mzalendoeditor