Featured Kitaifa

KAMATI YAPONGEZA UREJESHAJI WA FEDHA ZA MFUKO WA MAENDELEO YA VIJANA

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof.Joyce Ndalichako akiongoza Menejimenti ya Ofisi hiyo kuwasilisha randama ya mpango wa bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akijibu maswali katika Menejimenti ya Ofisi hiyo, ilipokuwa ikiwasilisha randama ya mpango wa bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii. Picha na OWM KVAU Machi 21, 2023.

Na Mwandishi Wetu Dodoma

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imepongeza Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa ufuatiliaji mzuri wa marejesho ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Pongezi hizo zimetolewa Machi 21, 2023 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Fatuma Toufiq katika kikao cha wasilisho la randama ya Mpango wa Bajeti Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kuhusu makadirio ya mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 kilichohudhuriwa na Waziri wa Ofisi hiyo Prof.Joyce Ndalichako na Menejimenti ya Ofisi hiyo.

Mhe. Toufiq amesema kamati inaridhishwa na urejeshwaji wa mikopo ya mfuko huo na kushauri utaratibu huo utumike kwenye mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango akiwasilisha kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Saidi Mabie amesema katika mbio za mwenge mwaka 2021/22 kiasi cha Sh.Bilioni mbili ambazo ni marejesho ya fedha za mfuko huo zilikusanywa.

Naye, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Prof. Jamal Katundu amesema wamewasilisha maombi ya nyongeza ya bajeti ya sh.Bilioni tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa Mwaka 2023/24.

Amebainisha kuwa kupitia Mfuko huo yamefanyika maboresho ya mwongozo wa utoaji mkopo wa mwaka 2022 ili kupanua wigo na kumuwezesha kijana mmoja mmoja kupata mkopo huku kiwango kikiongezeka kutoka Sh.Milioni 10 hadi 50.

About the author

mzalendoeditor