Featured Kitaifa

WAFANYAKAZI WANAWAKE ATC WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA KUHAMASISHA WASICHANA KUSOMA MASOMA YA SAYANSI.

Written by mzalendoeditor

NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Wafanyakazi wanawake wa chuo cha ufundi Arusha(ATC) wameadhimisha siku ya wanawake Duniani kwa kuwahamasisha wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Mateves iliyopo mkoani Arusha kusoma masomo ya sayansi ikiwa ni pamoja na kuwashauri juu ya mahusiano na kuwapelekea taulo za kike kwaaji ya kujisitiri wawapo katika siku hedhi.
Lucy Petro mmoja wa wafanyakazi wa chuo hicho alisema kuwa lengo kubwa la wao kutembelea shule hiyo ni kuwahamasisha wasichana kusoma masomo ya sayansi kwani wengi wana uwezo ila wanakosa msukumo kutokana na mazingira au jamii inayowazunguka yenye dhana potofu ya kuona kuwa waanawake kuna taaluma hawawezi kuwa nazo.
“Wamekuwa wakiona masomo ya sayansi kuwa ni masomo magumu na kufikiria kuwa hawawezi lakini uwezo wanao wanachokikosa ni ushauri na msukumo, lakini pia lengo lingine lililotuleta ni kuwajenga kiakili wajitambue wako wapi na wanakwenda wapi,” Alisema.
Rose Sadiki injinia wa umeme kutoka chuo hicho alisema yeye kama mwanamke amesoma masomo ya sayansi na anafanya kazi za kisayansi bila ugumu wowote hivyo aliwataka wasichana hao kutokuogopa kuchukua masomo ya sayansi kwani  kinachotakiwa ni kuyapenda pamoja na kusoma masomo kwa bidii.
“Mimi ningeogopa leo nisingekuwa hapa lakini nilithubutu na nikaweza sikujali dhana iyopo katika jamii kuwa ni masomo magumu  hivyo na nyie nataka msiogope, kunapokuwa na wanafunzi wa kwanza darasani wawili basi mmojawapo awe msichana, masomo haya sio magumu kama inavyosemekana ni kuongeza bidii tuu katika kusoma,” Alisema
Imelda Mdaba mfanyakazi wa ATC aliwataka wasichana hao kutojiingoza katika mahusiano ya kimapenzi wawapo shuleni badala yake wasome kwanza kwani katika umri wao hakuna kitu chochote ambacho mahusiano yatawasaidia zaidi ya kuharibu maisha yao.
“Hakikisha mtoto wa kike mwisho wa siku unafikia ndoto zako, jijue unataka kuwa nani na usome kwa bidii kwani ukiwa na elimu huwezi kukumbana na unyanyasaji wa kijinsi lakini pia niwasihi msiige mambo mabaya yasiyo na maadili yanayoendelea katika mitandao ya kijamii,” Aliwaeleza.
Alieleza kuwa mwanamke aliyesoma na kufanikiwa kufikia ndoto zake ana raha yake mojawapo ni kuvipata vile vitu vinavyoonekana vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa na mahusiano salama, simu nzuri na vitu vyote hivyo wajitengenezee mazingira mazuri wenyewe kwasasa kwa kusoma kwa bidii kwani elimu ndio kila kitu.
Atu Masawa mhasibu wa chuo hicho aliwataka wanafunzi hao kutojiingoza kwenye makundi mabaya badala yake waangalie  mbele yao kuliko leo kwa kuitengeneza leo kwani wakiondoka wamedanganyika watakuwa ni mzigo kwao peke yao, kwa familia na jamii kwa ujumla.
“Angalieni mbele yenu kwa tahadhari, yasitokee makundi ya ajabu hapa shuleni na wewe ukawa mmoja wapo, soma kwa bidii kuwa na nidhamu kwani ili baadae uje kuwa mama mzuri kwa watoto wako ni lazima leo yako iwe bora,” Alisema.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo Hadra Mwaja  mwanafunzi wa kidato cha tatu alisema kuwa kama wasichana wamekuwa wakipitia siku za mzunguko wa hedhi ambapo baadhi yao kutokana na kukosa vifaa vya kujisitiri kutoka na hali duni za kifamilia wamekuwa wakishindwa kuhudhuria masomo kwa siku kadhaa hivyo wanawashukuru wafanyakazi wanawake wa ATC kwa kuwaletea taulo za kike ambazo zitatatua changamoto hiyo kwa miezi kadhaa.
Makamu mkuu wa shule ya sekondari Mateves Edith Shuma alisema kumekuwa na utoro kwa watoto wa kike kutokana na kukosa vifaa vya kujisitiri wawapo katika siku zao hivyo wanashuru kwa kuleta taulo hizo ambazo zingine zimebaki katika ofisi za shule kwaajili ya kutumia pale inapotokea mwanafunzi akapata dharura ya kuingia katika siku zake bila kujijua.
“Lakini pia tunawashukuru kwa kuwahamasisha wasichana kusoma masomo ya sayansi na kuwapa elimu ya kike na niwaombe daraja hili mlilolijenga msiweke mpaka bali endeleeni nalo kwani utoro kwa watoto wa kike umekuwa ni mwingi kiasi wakati wakiwa kwenye siku zao,” alisema.

About the author

mzalendoeditor