Featured Kitaifa

WCF  YAFANIKIWA KULIPA MAFAO YA SH.BILIONI 44.61 KWA WANUFAIKA

Written by mzalendoeditor

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 2,2023 jijini Dodoma wakati akieleza utekelezaji wa majukumu ya Mfuko huo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Na.Alex Sonna-DODOMA

MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi nchini (WCF) umefanikiwa  kulipa mafao yenye thamani ya Sh. bilioni 44.61 kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko kubwa ukilinganisha na wakati kabla ya kuanzishwa kwake.

Hayo yamesemwa leo Machi 2,2023 leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Dkt. John Mduma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu  utekelezaji wa majukumu ya Mfuko huo.

“Hadi kufikia tarehe 30 Juni 2022, WCF imelipa mafao yenye thamani ya Sh. bilioni 44.61 kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko kubwa kwa kulinganisha na kipindi cha kabla ya kuanza kwa WCF ambapo malipo ya fidia yalikuwa chini ya Sh.milioni 200 kwa mwaka”amesema Dkt.Mduma

Aidha Dkt.Mduma amesema , kwa hesabu zisizokaguliwa, katika kipindi cha Julai 2022 hadi Desemba 2022, WCF ililipa mafao ya jumla ya Sh. bilioni 6.19 kwa wanufaika 1,004 na hivyo kufanya wanufaika wa Mfuko toka kuanzishwa kwake kufikia 10,454 ambao wamelipwa jumla ya Sh.bilioni 49.44.

“Kabla ya kuanzishwa kwa WCF, malipo ya fidia nchini kwa mwaka mzima yalikuwa chini ya Sh. milioni 200 lakini baada ya kuanzishwa kwa WCF  malipo yanaongezeka mwaka hadi mwaka hadi kufikia Sh. bilioni 9.3.  Serikali kupitia WCF imeleta mageuzi makubwa nchini,”amesema Dk. Mduma

Hata hivyo ameeleza kuwa katika takwimu za mwaka 2016/17, WCF ililipa fidia kwa wanufaika takribani 538 na kiasi cha Sh. milioni 613.84 kililipwa.

Aidha, amesema  kwa mwaka 2021/2022 pekee, WCF ililipa fidia kwa wanufaika takribani 1,600 na kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni 9.33 kililipwa.

Amesema kuwa , katika upande wa uwekezaji hadi kufikia tarehe 30 Juni 2022, Mfuko umekusanya jumla ya Shilingi bilioni 241.48 toka kwenye mapato yatokanayo na uwekezaji ambapo kwa takwimu za hivi karibuni, WCF ilitengeneza Shilingi bilioni 69.86 katika mwaka wa fedha 2020/2021 na Shilingi bilioni 74.29 katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Ameongeza  kuwa, jumla ya mali za Mfuko hadi Juni 30, 2022 ni Shilingi bilioni 545.16 ambapo asilimia 89.76 ya uwekezaji wa Mfuko upo kwenye Hati Fungani za Serikali.

About the author

mzalendoeditor