Featured Kitaifa

MAWAKALA WA FORODHA WAHIMIZWA UDHIBITI WA KEMIKALI HATARISHI

Written by mzalendoeditor

 

Mhandisi Goodluck Rulagora kutoka Chuo cha Uvuvi Bagamoyo (FETA) akitoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya vipimo sahihi vya kemikali vinavyotumika katika vifaa mbalimbali ikiwemo mitungi ya gesi kwa mawakala wa forodha wakati wa mafunzo ya siku. Mafunzo hayo yanaendeshwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku ya mbili kwa Mawakala wa Forodha wanaohusika na udhibiti na usimamizi wa kemikali na vifaa vya kemikali vinavyomong’onyoa tabaka la ozoni. Mafunzo hayo yanafanyika katika Ukumbi wa Taasisi za Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yanaendeshwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Washiriki wa mafunzo ya udhibiti na usimamizi na udhibiti wa kemikali na vifaa vya kemikali wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kwa mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoanza Machi 1, 2023 katika Ukumbi wa Taasisi za Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Jijini Dar es Salaam na kuendeshwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)

SERIKALI  imewataka mawakala wa forodha wanaoandaa nyaraka za kuingizia nchini na kupokea mizigo ikiwemo kemikali zinazodhibitiwa kuzingatia ukomo wa matumizi wa kemikali hizo zinazochangia mmong’onyo wa tabaka la ozoni na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi.

Wito huo umetolewa Machi 1, 2023) jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Catherine Bamwenzaki wakati akifungua mafunzo kwa mawakala wa forodha kuhusu udhibiti na usimamizi wa kemikali na vifaa vya kemikali vinavyomong’onyoa tabaka la ozoni.

Amebainisha kuwa kemikali au gesi zinazotumika katika mojokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto, usafirishaji chuma, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku, kuwa iwapo hatua hazitachukuliwa zinaweza kuingizwa nchini kupitia mipaka na kusababisha madhara kwa binadamu na mazingira.

Mhandisi Bamwenzaki amesema uchunguzi wa angahewa uliofanywa na wanasayansi umethibitisha kuwa Tabaka la Ozoni limekuwa likimong’onyoka kwa kasi ya asilimia tano (5) kila muongo ambapo matokeo ya uharibifu huo ni pamoja na kuruhusu mionzi zaidi ya urujuani kufika katika uso wa dunia.

Akifafanua zaidi Mhandisi Bamwenzaki amesema matokeo ya uvumbuzi huo yalisababisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) kufanya tathimini ya kisayansi na kuamua kuchukua hatua madhubuti katika kulinda tabaka hilo la Ozoni.

“Chini ya Programu ya Taifa, Serikali imeandaa na inatekeleza Mpango wa Kuondosha Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni ifikapo mwaka 2030 ambapo moja ya shughuli zinazotelekezwa ni pamoja na kutoa elimu kwa mawakala wa forodha na wasimamizi wa Sheria kuhusu Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za mwaka 2022” amesema Mhandisi Bamwenzaki.

Akiwasilisha Mada kuhusu Udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiewa chini ya Itifaki ya Montreal, Afisa Mwandamizi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Mhandisi George Ngoso amesema suala udhibiti wa kemikali na vifaa vya kemikali linahitaji nguvu ya pamoja vaina ya wadau waliopo katika mnyororo wa thamani ili kulinda afya za binadamu na mazingira.

Mhandisi Ngoso amesema ni wajibu wa mawakala wa forodha waliopo mipakani kujifunza teknolojia mpya ya ukaguzi wa mizigo ikiwemo bidhaa za kemikali kuendelea na usimamizi na udhibiti wa kemikali zinazodhibitiwa kwa kuzingatia ukomo wa matumizi wa kemikali hizo.

“Mnapaswa kuwa wazalendo na kutanguliza maslahi ya taifa na jamii inayowazunguka, madhara ya uingizaji wa bidhaa hizi unaweza kuleta athati kuwa kwa afya za binadamu  na mazingira, hivyo tunapaswa kuhakikisha kuwa tunadhibiti kemikali hizi kutoweza kuingia katika jamii yetu” amesema Ngoso.

Kwa upande wake Wakala wa Forodha kutoka Kampuni ya Freight Forwarders James Mramba ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendesha mafunzo hayo na kusema yataongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yao sehemu za kazi na kuhimiza mafunzo hayo kuwa endelevu ili kuwafikia wanufaika wengi zaidi.

“Naahidi kuwa Balozi kwa wenzangu kwa kushirikiana na watumishi wenzangu pamoja na taasisi nyingine za serikali ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na udhibiti wa kutosha wa uingizaji wa  kemikali ambazo zina athari kubwa kwa jamii na mazingira yetu” amesema Mramba.

Katika mafunzo hayo washiriki hao walielimishwa kuhusu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Kanuni za Kudhibiti Kemikali zinazoharibu Tabaka la Ozoni) za mwaka 2022, Udhibiti wa Uingizaji wa Kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itikafi ya Montreal, na Taratibu za maombi ya vibali vya usimamizi wa kemikali.

Jumla ya Mawakala wa forodha 25 walishiriki mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoanza Machi 01 hadi 03, 2023 na kuandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

About the author

mzalendoeditor