Featured Kitaifa

ZOEZI LA URASIMISHAJI MITAA 4 DODOMA KUANZA MACHI 6, 2023 

Written by mzalendoeditor

Meneja Urasimishaji Mjini Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Bw. Leons Mwenda akitoa elimu ya urasimishaji kwa Wananchi wa Mtaa wa Mapinduzi B Kata ya Ng’ong’ona wakati wa zoezi la uhamasishaji ngazi ya mtaa tarehe 1 Machi 2023 Jijini Dodoma

Diwani wa Kata ya Ng’ong’ona Mhe. Luth H. Luth akiongea na wananchi wa Mapinduzi B wakati wa zoezi la uhamasishaji lililofanyika tarehe 1 Machi 2023 Jijini Dodoma.

Mwananchi wa Mtaa wa Mapinduzi B, Kata ya Ng’ong’ona akichangia wakati wa zoezi la uhamasishaji ili kupata uelewa wa pamoja kabla ya urasimishaji kuanza tarehe 1 Machi 2023 Jijini Dodoma

Wananchi wa Mtaa wa Mapinduzi B, Kata ya Ng’ong’ona wakifuatilia kwa karibu semina ya uhamasishaji tarehe 1 Machi 2023 Jijini Dodoma.

Baadhi ya wanawake walioshiriki semina ya uhamasishaji katika Mtaa wa Mapinduzi B, Kata ya Ng’ong’ona wakifuatilia kwa karibu semina ya uhamasishaji tarehe 1 Machi 2023 Jijini Dodoma

Picha ya pamoja ya Kamati ya Urasimishaji Mtaa wa Mapinduzi B inayoongozwa na Diwani wa Kata ya Ng’ong’ona Mhe. Luth H. Luth (katikati) iliyochaguliwa na wananchi tarehe 1 Machi 2023 Jijini Dodoma

   

Na Magreth Lyimo, WANMM

Kazi za uwandani za urasimishaji makazi katika mitaa minne ya jiji la Dodoma zinatarajia kuanza rasmi Machi 6, 2023 baada ya kukamilika kwa kazi ya uhamasishaji wananchi ili kushiriki zoezi hilo.

Tayari zoezi la uhamasishaji limefanyika kwenye mitaa ya Mapinduzi A, Mapinduzi B katika Kata ya Ng’ong’ona, Mtaa wa Bihawana Kata ya Mbabala pamoja na Mtaa wa Mkwawa uliopo Kata ya Mpunguzi.

Hayo yamebainishwa na Meneja Mradi Urasimishaji Mjini, Bw. Leons Mwenda wakati wa zoezi la uhamasishaji wananchi kushiriki urasimishaji makazi katika Mtaa wa Mapinduzi B lililofanyika tarehe 1/3/2023 Jijini Dodoma.

Mwenda alisema, uhamasishaji ulifanyika katika ngazi ya Kitaifa, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kamati tatu za maendeleo ya Kata na sasa ni zamu ya wananchi katika ngazi ya mitaa lengo likiwa kuwapa uelewa wa pamoja wa kile kinachoenda kufanyika katika mitaa 4 ya jiji la Dodoma kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi.

‘‘Uhamasishaji umefanyika kwa mafanikio makubwa na katika mtaa huu wa Mapinduzi B zoezi la urasimishaji litaenda kuanza rasmi tarehe 6/3/2023 kwa kutambua, kupanga na kupima na mwisho mwananchi kupata hati miliki kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999’’ alisema Bw. Mwenda

Kwa mujibu wa Mwenda, zoezi hilo la urasimishaji litaenda kumuhusisha mwananchi moja kwa moja katika kila hatua ili kila mmoja awe na uhakika wa kile kinachofanyika ili kuepuka migongano isiyo ya lazima.

‘‘Urasimishaji ni mpango shirikishi wenye lengo la kutambua, kupanga, kupima na kumilikisha ardhi iliyojengwa bila kupangwa, na kauli mbiu ni tupange Miji yetu kwa pamoja ambapo kazi za uwandani zinatarajiwa kukamilika ndani ya miezi minne ili kutoa fursa ya wananchi kupatiwa hati miliki za ardhi yao’’ alisisitiza Bw. Mwenda

Naye Diwani wa Kata ya Ng’ong’ona Mhe. Loth H. Loth alisema kuwa, ardhi ndio uti wa mgongo wa wananchi hivyo mradi huu una manufaa kwa wananchi kwa kuwa ameufuatilia kwa karibu na kuona utekelezaji wake utakavyokuwa na kuwataka wananchi wa Mapinduzi B kuupokea mradi huo pamoja na kuwapa ushirikiano wataalamu watakaokwenda kutekeleza zoezi la urasimishaji.

Kwa upande wake Afisa Mipango Miji kutoka Jiji la Dodoma Bi. Anna Nade alisema kuwa, kupanga matumizi ya ardhi ni sehemu muhimu sana katika kuleta maendeleo ya mji hivyo wananchi kupitia mradi huo wa urasimishaji wanapaswa kupanga matumizi ya ardhi ya maeneo yao ambapo alitolea mfano wa viwanja vya makazi au vya biashara lakini pia alielimisha umuhimu wa kutenga barabara alizozieleza kuwa zitachagiza kuleta maendeleo ya kiuchumi katika maeneo yao.

Katika kikao hicho wananchi walipata fursa ya kuchangia ambapo walisema kuwa mradi huo utawasaidia kupata hati walizozieleza kuwa zitawaongezea sifa katika kupata mikopo kwenye taasisi za fedha na kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi ni mradi unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa muda wa miaka mitano ukiwa na dhumuni la kuongeza usalama wa milki kwa kutoa hati miliki 2,000,000 pamoja na hati miliki za kimila 500,000. Mradi pia utajenga ofisi za ardhi katika mikoa 25 ili kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya utunzaji taarifa za ardhi pamoja na ukarabati wa
ofisi za ardhi katika Halmashauri 41 nchini.

About the author

mzalendoeditor