Featured Kitaifa

ASKOFU KINYAIYA AKERWA NA MMOMONYOKO WA MAADILI KWA VIJANA

Written by mzalendoeditor

Wanautume wa Utume wa Fatima wakiwa katika Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi wa Utume huo Jimboni Dodoma,katika Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska-Kiwanja cha Ndege.

Viongozi wa Utume wa Fatima Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma wakiwa katika picha ya pamoja na Mhashamu Beatus Michael  Kinyaiya mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi wa Utume huo.

Wanakwaya wa Kwaya ya Shirikisho Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska-Kiwanja cha Ndege,wakiinjilisha kwa njia ya uimbaji wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi wa Utume wa Fatima Jimboni Dodoma.(Picha zote na Ndahani Lugunya).

Na Ndahani Lugunya,Dodoma.

Askofu Mkuu Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael  Kinyaiya amesema kuwa,pamoja na kuepo kwa watu wenye uhitaji wa chakula na mavazi katika jamii,Vijana nao ni miongoni mwa kundi la watu wenye uhitaji kwani wamezongwa na wimbi kubwa la mmomonyoko wa maadili.

Amesema hayo wakati akitoa homilia yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi wa Utume wa Fatima katika Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma,misa iliyofanyika katika Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska-Kiwanja cha Ndege Jimboni Dodoma.

“Katika jamii tunayoishi ina watu wengi wanaohitaji labda sio nguo na mavazi tu kivile lakini tunapo tazama tunaona kuna shida kuna changamoto tunaona mmomonyoko wa maadili ndio watu wanaohitaji kusaidiwa.mmonyonyoko wa maadili kwa vijana ndio watu wenye kiu wanao hitaji kupewa maji hawa,” amesema Askofu Kinyaiya.

Hata hivyo katika suala hilo la maadili kwa Vijana,Askofu Mkuu Kinyaiya amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hasani na Makamu wake Dkt Filipo Isdor Mpango,kwa kuendelea kukemea suala la mmomonyoko wa maadili kila wanapotoa hotuba zao.

“Sasa nawewe kwa upande wako umechangia nini katika hilo kama hawa Viongozi wetu? wewe mzazi umekwisha kaa chini na kijana wako mkaongea ukamueleza madhara ya mambo anayo yafanya,iwe ni suala la utandawazi kama kuangalia picha zisizokuwa na maana,ulevi na utumiaji wa bangi.umekwisha kaa chini ukamwambia kijana wangu acha hii kitu starehe hizo zitakupeleka pabaya,tumeshafanya hivyo wazazi?.

Au tunasema huyu ni mtu mzima bhana achana nae,jamani mtoto kwa mzazi hakui wazazi naomba mnielewe mtoto kwa mzazi hakui hata siku moja,una wajibu wa kukaa na mtoto wako umfundishe madhara ya vitu anavyo vifanya,” amesema Askofu Kinyaiya.

Aidha pamoja na wazazi amewataka walezi wakiwemo walimu waliokabidhiwa watoto shuleni kuanzia ngazi ya awali hadi Shule za Sekondari

kutambua kwamba wao ndio wazazi wa watoto hao,na hivyo kila mmoja ajiulize anachukua jitihada gani kukabiliana na mmomonyoko wa maadili ambapo kwa sasa katika maeneo ya mashuleni ndiko umeshika kasi.

Askofu Mkuu Kinyaiya amesema walimu wakiwa kama walezi wa watoto mashuleni wana kila sababu ya kuchukua hatua madhubuti kukabiliana  na mmomonyoko wa maadili bila kujali Shule walizopo ni za Dini au Serikali,na kwa hivyo lazima walimu wawajibike ipasavyo katika hilo.

“Suala la maadili halina mipaka,hakuna cha Serikali,Dini au Kanisa bali wote tuna husika kumbe naomba tuwatazame hawa wahitaji wetu tuwashauri na tuwasaidie,” amesema Askofu Kinyaiya.

Akizungumzia kuhusu utume wa Fatima Askofu Kinyaiya amesema kwamba,uzinduzi rasmi wa utume huo iwe chachu kwa waamini wote kuwa tone la chumvi katika dunia na kuwa mwanga ili watu waweze kuona na kumtambua Kristo.

“Tunawapongezeni sana ndugu zangu kwa ujasiri huo na karibuni sana.wote nawaombea tuwaombee hawa lakini tuwasiwaombee tu nenda kajitafakari ili nawewe kwanza usiwe gunia la chumvi na mbili mpende Mama Maria usali Rozali na ufanye toba,”  amesema Askofu Kinyaiya.

Awali katika utangulizi wa Adhimisho la Misa Takatifu,Paroko wa Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska-Kiwanja cha Ndege Padri Emmanuel Mutambo,amesema kuwa  chama cha Utume wa Fatima kilianzishwa mwaka 1947 Amerika ya Kaskazini  kikiwa na malengo mbalimbali ya uinjilishaji.

“Madhumuni ya Utume wa Fatima ni kuchochea mafundisho ya kweli ya Kanisa Katoliki na kutetea kikamilifu mafundisho ya Injiili,kuwatakatifuza wana utume wa Fatima na kuutakatifuza ulimwengu kufuata kiaminifu ujumbe wa Fatima na mwisho ni kuhakikisha kuwa jitihada zinafanywa kufikisha Ujuumbe wa Fatima kwa watu wote” ameeleza Askofu Kinyaiya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Utume wa Fatima Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Magreth Joji Kaulananga,amesema Utume wa Fatima una jukumu la kueneza na kuishi ujumbe wa Mama Bikira Maria alioutoa Fatima nchini Ureno mwaka 1917 kwa watoto watatu wachungaji yaani Lucia,Fransis na Yasinta.

“Mama Maria alipotokea  kule Fatima alihimiza kwamba watu tusali Rozali tujitolee nafsi zetu yaani kutoa sadaka,kujitolea kwa moyo wake safi ili tunapofanya hayo yote dunia iweze kupata amani.

Tukumbuke kwamba mwaka 1917 wakati Mama Bikira Maria anatokea ulimwengu au dunia ilikuwa inakabiliwa na kitisho cha Vita kuu ya kwanza ya dunia ambapo watu walikuwa wakipoteza maisha na wengi roho zao zilikuwa zinaingia motoni na zingine toharani.

Kumbe Mama Bikira Maria anakuja duniani kutuletea ujumbe wa wokovu na ujumbe wenyewe ni rahisi sana kuutekeleza,kubwa ni kusali Rozali,kujitolea magumu,kufanya sadaka kwa ajili ya kuutuliza moyo mtakatifu wa Yesu kwa nia ya kuleta amani duniani na wongofu wa roho za wakosefu na hata wale walioko toharani waweze kuokolewa,” amesema  Kaulananga.

Utume wa Fatima Jimboni Dodoma hadi sasa una wanautume ambao wapo katika Parokia 11 za Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma,ambazo ni pamoja na Hembahemba,Ihumwa,Nzuguni,Ilazo,Kiwanja cha     Ndege,Chidachi,Veyula,Swaswa,Kanisa Kuu,Kongwa  na Kibaigwa.

About the author

mzalendoeditor