Featured Michezo

UWANJA WA MKAPA KUFANYIWA MABORESHO MAKUBWA KWA AJILI YA MICHUANO YA AFRIKA SUPER LEAGUE

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu akizungumza na Uongozi wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ( CAF) ulioongozwa Bw. Mohamed Sidat, Mkuu wa Kitengo Cha Ufundi, Februari 16,2023 jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu akiwa Katika picha ya pamoja na Uongozi wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ( CAF) ulioongozwa Bw. Mohamed Sidat, Mkuu wa Kitengo Cha Ufundi, Februari 16,2023 jijini Dar es Salaam

Serikali imeahidi kufanya marekebisho makubwa yanayohitajika katika uwanja wa Benjamin Mkapa ili kukidhi viwango vya kimataifa vinavyohitajika katika michuano ya Africa Super League ambayo Klabu ya Simba ndio mwakalishi wa ukanda wa Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa Februari 16, 2023 jijini Dar es Salaam na Bwana Saidi Yakubu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo alipokutana na uongozi wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) ambao unaongozwa na Bw.Mohammad Sidat,Mkuu wa Kitengo cha ufundi alieambatana na wataalaam kutoka Italia waliokodiwa na Shirikisho hilo.

Bwana Yakubu alieleza kuwa maeneo yote yaliyoainishwa yatafanyiwa kazi kabla ya ziara nyingine ya ukaguzi itakayofanywa na CAF.

Aidha,Bwana Yakubu pia aliwaeleza viongozi hao kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inakusudia kujenga viwanja vingine vya michezo na watategemea sana miongozo ya kitaalamu toka FIFA na CAF.

Kwa upande wao,Ujumbe huo wa CAF waliarifu kuhusu hatua za haraka zinazotakiwa kufanywa ili uwanja uendelee kutumika kimataifa na kupongeza maendeleo ya soka nchini.

Uongozi wa klabu ya Simba uliandaa hafla hiyo ya chakula cha jioni iliyohudhuriwa pia na Naibu Spika,Mussa Azzan Zungu kwa nia ya kufanya tathmini baada ya ukaguzi kufanyika.

About the author

mzalendoeditor