Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS ATETA NA MKURUGENZI WA LONGPING YA CHINA

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Longping Agriscience LTD wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Liang Shi, mazungumzo yaliofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam leo tarehe 17 Februari 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Kampuni ya Longping Agriscience LTD wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Liang Shi pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde mara baada ya mazungumzo yaliofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam leo tarehe 17 Februari 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Longping Agriscience LTD Liang Shi mara baada ya mazungumzo yaliofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam leo tarehe 17 Februari 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 17 Februari 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni inayojishughulisha na Kilimo kutoka nchini China ya Longping Agriscience LTD wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Bwana Liang Shi, Mazungumzo yaliofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam.

Katika Mazungumzo hayo, Makamu wa Rais ameipongeza kampuni hiyo kwa nia yake ya dhati ya kuwekeza katika kilimo hapa nchini kwa kutambua uhusiano wa muda mrefu baina ya Tanzania na China. Amesema Tanzania inaendelea na jitihada za kuimarisha sekta ya kilimo ikiwemo kuanzisha programu ya kilimo biashara (Building Better Tomorrow) yenye lengo la kuwasaidia vijana kushiriki katika sekta hiyo kikamilifu na kuchochochea ukuaji wake kufikia lengo la asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. 

Makamu wa Rais amesema ushirikiano huo utaongeza mafanikio zaidi katika kuifanya Tanzania kuwa nchi tegemeo kwa chakula Barani Afrika kwa kuzingatia uwepo wa ardhi nzuri ya kilimo pamoja na jiographia ya kuvutia. Aidha ameongeza kwamba malengo ya kampuni hiyo katika kuweka mnyororo wa thamani kuanzia uzalishaji wa mbegu hadi uzalishaji mazao na uongezaji thamani wa mazao hayo viwandani, utaweza kuongeza tija katika kilimo hapa nchini.

Halikadhalika amewasisitiza kutumia ubunifu, utafiti, ulinzi wa mimea na matumizi ya teknolojia rafiki ili kuongeza uzalishaji. Pia kutoa mafunzo na vitendea kazi kwa wakulima na kutumia vema ardhi watakayopata kwa maendeleo endelevu.

Kwa upande Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Longping Agriscience LTD bwana Liang Shi amesema Tanzania ni nchi nzuri yenye ardhi ya rutuba iliobarikiwa kuwa na idadi ya watu ya kutosha pamoja na jiographia itakayosaidia uzalishaji wa mazao wa uhakika utakaopelekea Tanzania kuwa tegemeo la chakula kwa Afrika na Dunia kwa ujumla.

Amesema kampuni hiyo imelenga kuanzisha mashamba ya darasa, kuwasaidia wakulima wazawa kwa mafunzo ya vitendo, kuanzisha vituo vya mauzo vitakavyoweka uwazi wa bei za mazao katika maeneo mbalimbali nchini.

About the author

mzalendoeditor