Featured Kitaifa

SERIKALI KUONGEZA WIGO KASI YA MAWASILIANO KUTOKA 45% KUFIKIA 80%

Written by mzalendoeditor
 Naibu waziri ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala Bora Deogratius Ndejembi akifungua kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao unaoendelea mkoani Arusha.
mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya serikali mtandao (e-GA) mhandisi Benedict Ndomba  akieleza majukumu ya mamlaka hiyo pamoja na mafanikio ya mamlaka.
KATIBU Mkuu ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Laurence Ndumbaro akiongea katika kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao unaoendelea mkoani Arusha
………………………………..
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA

Naibu waziri ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala Bora Deogratius Ndejembi amesema kuwa serikali imejipanga kuongeza wigo wa mawasiliano ya kasi kutoka asilimia 45 iliyopo sasa hadi kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2025.

Ndejembi ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao (e-GA) unaoendelea mkoani Arusha ambapo amesema kuwa kupitia TEHAMA Dunia hivi sasa imekuwa ni Kijiji hivyo pamoja wigo huo pia imejipanga kuongeza kasi ya kufikisha miundombinu ya mkongo wa taifa kwenye maeneo mengi nchini hususan katika ngazi za wilaya.
“Katika Dunia ya kiuchumi tuliyopo sasa TEHAMA ni nyenzo wezeshi, na kwa umuhimu huu serikali  imewekeza na kuweka kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA kupitia mamlaka ya serikali mtandao  kwa kujenga miundombinu ya mfumo tumizi  na kisekta ili kusaidia kuboresha ufanisi na uendeshaji wa shughuli zake,” alisema Ndejembi.
Aidha aliitaka mamlaka ya serikali mtandao (e-GA) kuendelea kufanya tafiti ili kuweza kuleta bunifu ya mifumo ya TEHAMA itayoliwezesha taifa kufanikisha kuimarisha sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji pamoja na kulipekeka taifa mbele kimaendeleo.
Alisema serikali ya awamu ya sita chini  Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu, wakati akihutubia bunge kwa mara ya kwanza alieleza bayana kuwa serikali yake itatoa kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA hususan katika masuala ya utafiti na ubunifu ili kuweza kuimarisha usalama wa mtandao wa mawasiliano, kuongeza watumiaji wengi kutoka asilimia 43 na kuweza kufikia asilimia 80 ifikapo 2025.
“Ili kutimiza azma hiyo ya Mh Rais nitoe wito kwenye ninyi washiriki kutoa maoni yenu, ushauri na mapendekezo katika kikao hiki  yatayowezesha serikali kutekeleza jitihada za serikali mtandao wenye tija, ufanisi na zinazoboresha utoaji wa huduma bora kwa umma pamoja na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa letu,” Alieleza Ndejembi.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya serikali mtandao (e-GA) mhandisi Benedict Ndomba alieleza kuwa mamlaka hiyo inaendelea kusimamia na kuhimiza uzingatiaji wa sera, sheria, kanuni, viwango na miongozo ya serikali mtandao kwa taasisi za umma ambapo wameendea kutoa miongozo mbalimbali ya kiufundi ili kuhakikisha kuwa matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma yanakuwa na tija ikiwemo kusaidia katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma.
“Katika kipindi hiki tumetekeleza jukumu la kufanya ukaguzi wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA na kutoaa ushauri wa kitaalamu kuhusu matumizi sahihi na salama ya TEHAMA serikalini ili kuhakikisha usalama wa mifumo na katika kutekeleza jukumu hili tumeweza kubaini matishio ya kiusalama mtandaoni yapatayo 459 sambamba na kufanya kaguzi na tathimini za usalama wa mifumo katika taasisi za umma,” alifafanua Mhandisi Ndomba.
Alisema mpaka sasa mamlaka imetengeneza zaidi ya tovuti 300, kuunganisha taasisi za serikali 394 kutoka sekta mbalimbali katika mtandao wa serikali ambao ni salama na gharama nafuu lakini pia wameweza kutoa masafa ya intanet kwa taasisi za umma 554.
Naye katibu mkuu ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Laurence Ndumbaro aliwataka watumishi wa sekta hiyo kujitahidi kuhuisha tovuti zao ziweze kuwa na taarifa zinazoenda na wakati na kuendana na teknolojia ya kisasa ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya karatasi.

About the author

mzalendoeditor