Featured Kitaifa

NSSF KUKUSANYA MICHANGO YA SH.TRILIONI 1.6

Written by mzalendoeditor

WAANDISHI wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi  Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)Masha Mshomba, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mfuko na mwelekeo wa utendaji katika mwaka wa fedha 2022/23 leo Februari 8,2023 jijini Dodoma

MKURUGEZI Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)Masha Mshomba,akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 8,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mfuko na mwelekeo wa utendaji katika mwaka wa fedha 2022/23.

………………………..

Na.Alex Sonna-DODOMA

MKURUGEZI Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)Masha Mshomba,amesema  katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2023, mfuko huo unatarajia kukusanya michango ya shilingi trilioni 1.6 ambayo ni ongezeko la asilimia 14 ukilinganisha na michango ya shilingi trilioni 1.4 iliyokusanywa na Mfuko katika mwaka wa fedha ulioishia mwezi Juni 2022.

Hayo ameyasema leo Februari 8,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mfuko na mwelekeo wa utendaji katika mwaka wa fedha 2022/23.

Amesema Mfuko umeendelea kuimarisha mifumo na usimamizi wa fedha ili kuepuka mianya ya upotevu wa fedha, kuendelea kumudu gharama za uendeshaji pamoja na kulipa mafao stahiki kwa wastaafu na wanufaika wengine.

“Katika mwaka wa fedha 2022/23, Mfuko umeendelea kuimarisha mifumo na usimamizi wa fedha ili kuepuka mianya ya upotevu wa fedha, kuendelea kumudu gharama za uendeshaji pamoja na kulipa mafao stahiki kwa wastaafu na wanufaika wengine,
“Katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2023, Mfuko unatarajia kulipa mafao yenye thamani ya shilingi bilioni 769.3 ambayo ni ongezeko la asilimia 17 ukilinganisha na shilingi bilioni 659.8 zilizolipwa katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2022,”amesema Mshomba
Bw.Msomba amefafanua kuwa hadi kufikia Julai mosi mwaka huu tayari itakuwa imeweza kuzalisha sukari kupitia kiwanda cha sukari cha Mkulazi.
Kiwanda hicho kimeelezwa kuwa kitapunguza changamoto ya uhaba wa sukari inayojitokeza mara kwa mara na kulazimu serikali kutegemea wazalishaji na waagizaji binafsi kuzalisha na kuagiza sukari.
“Mradi huu unatarajiwa kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka na umefikia asilimia 75 na unatarajiwa kukamilika katika mwaka huu wa fedha na uzalishaji wa sukari kuanza Julai, 2023,”amesema Mshomba.
Mshomba amesema kuwa Mradi huo unatarajiwa kutoa fursa ya soko kwa wakulima wa nje wanaolima miwa katika mashamba yenye takribani hekta 450, miundombinu mingine kwa ajili ya wananchi wanaouzunguka mradi huo,ajira zaidi ya 2,315 za moja kwa moja, megawati 15 za umeme zinazotarajiwa kuingizwa katika gridi ya Taifa kupitia kituo cha kupokelea na kupoza umeme Msamvu.
Aidha ametaja mafanikio ya mfuko huo ni kuwa ukuaji wa Mfuko kwa Kiwango Kikubwa Katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mfuko umekuwa kwa kiasi kikubwa ambapo thamani ya Mfuko imeongezeka na kufikia shilingi trilioni 6.6 mwezi Desemba 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 39 kutoka shilingi trilioni 4.7 iliyofikiwa mwezi Machi 2021.

About the author

mzalendoeditor