Featured Kitaifa

VIONGOZI WA UMMA WAASWA KUWA NA MAADILI

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebecca Sanga akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya maadili kwa Viongozi wa Umma wa mkoa wa Morogoro.Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Hazina ndogo mkoani Morogoro tarehe 07 Februari, 2023. Kulia kwa Mhe. Sanga ni Katibu Msaidizi  Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma  kanda ya Mashariki-Morogoro Bw. Henry Sawe na Kushoto kwa Mhe. Sanga ni Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili  ya Viongozi wa Umma Idara ya Ukuzaji maadili makao makuu-Dodoma Bw. Salvatory Kilasara.

Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya  Mashariki Bw. Henry Sawe akitoa neno la ufunguzi katika mafunzo ya Maadili  kwa  Viongozi  wa umma yaliyofanyika katika ukumbi wa Hazina ndogo mkoani Morogoro tarehe 07 Februari, 2023.Wengine katika picha ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebecca Sanga (katikati) akifuatiwa na Katibu Msaidizi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma  Idara ya Ukuzaji Maadili Makao makuu-Dodoma Bw. Salvatory Kilasara. 

Afisa kutoka Sekretarieti ya Maadili  ya Viongozi wa Umma  kanda ya Mashariki- Morogoro Bi. Zainab Kissoky akitoa mada kuhusu Sheria ya Maadili ya Viogozi wa Umma Na.13 ya mwaka 1995, katika mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma yaliyofanyika katika ukumbi wa Hazina ndogo mkoani Morogoro  tarehe 07 Februari ,2023.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebecca Sanga (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma mkoani Morogoro,yaliyofanyika katika Ukumbi wa Hazina ndogo mkoani Morogoro tarehe 07 Februari,2023. Kushoto kwa Mhe. Sanga ni Katibu Msaidizi  Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Mashariki- Morogoro Bw. Henry Sawe na kulia kwa Mhe. Sanga ni Katibu Msaidizi   Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Idara ya Ukuzaji Maadili Makao Makuu-Dodoma Bw. Salvatory Kilasara.

…………………………

Viongozi wa Umma nchini waaswa kuwa na maadili mema katika utendaji kazi wao wa kila siku ili kuleta tija katika jamii na kwa taifa kwa ujumla

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebecca Sanga alipokua akifungua mafunzo ya  Maadili kwa Viongozi wa Umma kutoka Taasisi, Idara na Mashirika ya Umma Mkoani Morogoro. Mafunzo hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Hazina ndogo mkoani Morogoro tarehe 07 Februari, 2023.

Akifungua mafunzo hayo Mhe.Sanga alisema kuwa maadili  ni  nyenzo muhimu sana kwa kila kiongozi kuwa nayo, maadili ni  dhana pana inayojumuisha ; mwenendo mwema, mambo ya haki, usawa na mafundisho mema na ndio kiini cha kufanikiwa kwa maendeleo ya sekta mbalimbali za kijamii kama elimu , maji, umeme na nyingine nyingi.

Mhe. Sanga alieleza kuwa kila kiongozi yeyote wa Umma anapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia  maadili  kwani kiongozi ni kioo cha jamii  yoyote ile hivyo kiongozi  anapokua na maadili hawez kufanya mambo ambayo ni kinyume na taratibu, sheria na miongozo mbalimbali iliyowekwa nchini  kama vile  kutokutoa ama kupokea rushwa, ukiukwaji wa haki za binadamu, kujiingiza katika mgongano wa maslahi, pamoja na taratibu nyingine jambo ambalo litawafanya wananchi kuwa na imani na serikali yao “Maadili ni kinga dhidi ya maovu yote”alisema.

Mhe. Sanga alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia  Suluhu Hassan inasisitiza Viongozi kuwa na maadili mema ,  viongozi kuwa na tabia na mienendo isiyotia shaka, viongozi kutokua na dosari za kimaadili  hivyo viongozi wote wanapaswa kuwa na maadili mazuri ili kwenda sanjari na dhamira ya serikali “Niwaase viongozi wenzangu kuwa wakati wote uadilifu uwe kipaumbele katika maisha ya kila siku tukiwa kazini ama nje ya mahala pa kazi” alisema.

Aidha Mhe. Sanga alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Viongozi maelekezo mbalimbali  ya serikali yanayohusu maadili ikiwa ni pamoja na: Kiongozi   kutanguliza maslah ya umma mbele badala ya maslah binafsi, Kiongozi  kutanguliza uzalendo na maslah ya Umma mbele kwa ajili ya maendeleo ya Taifa  katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, Kiongozi  kuzingatia maadili,  nidhamu katika kazi, kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya rushwa , kuzingatia  haki za binadamu, kuwa na uwazi katika utendaji kazi na mengine mengi.

Pamoja na hayo Mhe. Sanga alieleza kuwa mafunzo hayo kwa viongozi wa umma yatasaidia kuwajenga kimaadili na kuwakumbusha umuhimu wa kuzingatia misingi ya maadili wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku  na ni  sehemu ya mikakati ya kuwajengea uwezo wadau mbalimbali ambao ni pamoja na Viongozi wa Umma ambao   kimsingi ndio wanaohusika na utekelezaji wa shughuli za serikali lakini pia ni wasimamizi wa rasilimali za umma.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Katibu Msaidizi  Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Mashariki Bw. Henry Sawe alisema kuwa mafunzo hayo kwa viongozi wa umma ni hatua muhimu katika jitihada za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kusimamia na kukuza maadili nchini.

Bw. Sawe alieleza kuwa jitihada hizo  zinakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa tunakua na Taifa lililojengwa juu ya misingi na mifumo ya maadili. “sote tunafahamu kwamba Serikali yetu imekua wakati wote ikiweka uzito unaostahili katika suala la kusimamia na kukuza uadilifu nchini.

Katika mafunzo hayo ya siku moja mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na  Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 pamoja na kanuni zake, Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi na Watumishi wa Umma, Tamko la Rasilimali na Madeni, Mgongano wa Maslahi kwa Viongozi na Watumishi wa Umma, pamoja na uwajibikaji katika utumishi wa Umma.

About the author

mzalendoeditor